DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia kituo chake cha IMF AFRITAC East kwa kuchangia ustawishaji wa uchumi wa Tanzania kupitia programu mbalimbali za mafunzo na ushauri.Amesema, mchango huo unaisaidia BoT katika utekelezaji wa sera ya fedha kwa ufanisi na kuimarisha sekta ya fedha nchini.
Gavana Tutuba ametoa shukrani hizo Septemba 10, 2024 alipokutana na Mkurugenzi wa IMF AFRITAC East, Bi. Clara Mira, ambaye ameteuliwa hivi karibuni.
“Nachukua fursa hii kuishukuru IMF AFRITAC East kwa jitihada endelevu za kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Benki Kuu ambazo zimesaidia kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kustawisha sekta ya fedha,” amesema Gavana Tutuba.
Aidha, amemueleza Mkurugenzi huyo kuwa uchumi wa Tanzania umeimarika licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na misukosuko kadhaa ya kidunia.
Ameongeza kuwa maoteo ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2024 ni kufikia asilimia 5.6 ikiwa ni ongezeko la ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023.
“Maotoe haya yanatokana na mikakati mbalimbali ya uboreshaji iliyofanywa na Serikali ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini, kukuza uwekezaji, kuimarika kwa hali ya uchumi wa dunia na upatikanaji wa mikopo kupitia program ya Extend Credit Facility (ECF) na dirisha la Mfuko wa Ustahimilivu na Uhimilivu (Resilient and Sustainable Fund-RSF),” amesema Gavana huyo.