NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Tanzania imeufahamisha umma kuwa,imechapisha Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024 (Guidance Note on Digital Lenders Under Tier 2 Microfinance Service Providers, 2024).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 24, 2024 na Naibu Gavana,Dkt. Yamungu M. Kayandabila imefafanua kuwa, mwongozo huo unalenga kuimarisha usimamizi wa uendeshaji wa huduma za mikopo kidijitali kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili nchini.
Aidha, Mwongozo huu unalenga kuhakikisha uzingatiwaji wa kanuni za kumlinda mlaji wa huduma za kifedha, ikijumuisha uwazi, uwekaji wa bei, njia za ukusanyaji wa madeni, utunzaji wa taarifa binafsi za wateja na faragha.
Kufuatia kutolewa kwa Mwongozo huu, Benki Kuu ya Tanzania inawaelekeza Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa au wanaokusudia kutoa mikopo ya kidijitali kutii matakwa ya Mwongozo huu.
Endapo mtoa huduma atakiuka agizo hili, Benki Kuu itachukua hatua za kiutawala, ikiwemo faini, kusitisha shughuli za utoaji mikopo ya kidijitali, na kufutiwa leseni ya kuendesha biashara ya huduma ndogo za fedha.
Benki Kuu itachapisha na kuhuisha orodha ya watoa huduma walioidhinishwa kutoa huduma za kidijitali katika tovuti yake. Mwongozo huu unapatikana kupitia tovuti ya Benki Kuu: https://www.bot.go.tz/Publications/Acts,%20Regulations,%20Circulars,%20Guideline s/Guidelines/en/2024082813141188.pdf