Boti hii ya doria itumike kwa kuzingatia mwongozo uliopo-Dkt.Yonazi

DAR-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara za magendo na utoroshaji wa nyara za serikali katika Bahari na Maziwa yote nchini.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi (katikati) akikabidhi mfano wa ufunguo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirikia la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Mohamed Salum wakati wa hafla ya makabidhiano ya boti ya doria (PB SAILFISH) kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na shirika hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 19, 2024 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati wa hafla ya makabidhiano ya Boti ya Doria (PB SAILFISH) iliyofanyika katika Chuo cha Bahari (DMI) Jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Yonazi amesema, lengo kuu la kununuliwa kwa boti hiyo ni kuimarisha doria ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu nchini, hivyo, boti hiyo itatimiza lengo na kuimarisha juhudi za Serikali za kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika eneo lote la bahari.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya boti ya doria (PB SAILFISH) kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

“Ni matumaini ya serikali kuona boti hii inatumika ipasavyo katika shughuli zilizopangwa na zitakazojitokeza kwa mujibu wa mahitaji ya matumizi kwa wakati husika. Aidha, naomba kuwasisitizia kuwa matumizi ya boti hii pia yazingatie Mwongozo wa Kitaifa wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu wa mwaka 2022,” amesema Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi amewataka wadau na mashirika kuendelea kufanya kazi na Idara ya Menejimenti ya Maafa iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kuweza kuratibu programu za uokozi kwa majanga ya majini na usalama wa bahari kwa ujumla na kuwashukuru wafadhili kwa ufadhili na ushirikiano walioutoa wakati wa ununuzi wa boti hiyo.

“Ninaomba kutumia nafasi hii kuwajulisha kuwa, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ina imani kubwa na uwezo wa TASAC katika usimamizi, uendeshaji na utunzaji wa boti hii, hiyo ndiyo sababu iliyopelekea boti hii kukabidhiwa kwa shirika hili. Ni imani yetu kuwa mtaitunza vizuri ikiwa ni pamoja na kuifanyia matengenezo kinga kwa wakati na hivyo kuwaongezea ufanisi katika kazi zenu za kila siku hususani katika ukaguzi kwa meli zinazoingia kwenye maji yetu ya ndani,” amesema Dkt.Yonazi.
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) waliohudhuria Hafla ya Makabidhiano ya Boti ya Doria (PB SAILFISH).
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Bw. Ludovick Nduhiye amesema, boti hiyo itakuwa ni jibu katika utekelezaji wa malengo na jitihada zinazofanywa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na wadau wa sekta ndogo ya usafirishaji majini katika kudhibiti wa vitendo vya kiuhalifu katika maeneo ya mwambao wa bahari na Maziwa Makuu.

“Kukabidhiwa kwa boti hii kwa Shirika letu la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imekuwa chachu katika kutimiza kwa vitendo Dira yetu ambayo imelenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye huduma za uchukuzi na hali ya hewa yenye uhakika, usalama na nafuu,” amesema Bw. Nduhiye.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirikia la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum akitoa neno la ufunguzi katika hafla ya makabidhiano ya boti ya doria (PB SAILFISH) kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

Kwa upande wake Mkuu wa Shirikia la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),Bw. Mohamed Salum ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wananendelea na shughuli zao majini wakiwa katika hali ya usalama, aidha amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Mjaliwa kwa kuweka msukumo ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ambao ni matokeo ya boti hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news