BRELA yawashauri wabunifu wa maumbo na michoro kufanya bunifu zenye mvuto wa kipekee

DAR-Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewashauri wabunifu, watafiti, wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, wasanifu majengo na wajasiriamali kubuni Michoro na Maumbo yenye mvuto na upekee wanayotumia kwenye biashara zao kama vile vifungashio/mikebe, michoro ili kuvutia walaji na watumiaji wa bidhaa na huduma na kuhakikisha bunifu hizo zinalindwa kisheria.
Wito huo umetolewa leo na Bw. Godfrey Nyaisa, Afisa Mtendaji Mkuu kutoka BRELA katika kikao cha mashauriano ya wadau kuhusu rasimu ya Mkataba wa Sheria ya Maumbo na Michoro Bunifu iliyoandaliwa chini ya Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (World Intellectual Property Organization-WIPO).

Kikao hicho ni maandalizi ya uidhinishwaji wa sheria hiyo ya kimataifa katika mkutano wa Kidiplomasia unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2024 Riyadh nchini Saudi Arabia.
Akifungua majadiliano, Bw. Nyaisa amesema kuwa Mkataba wa WIPO wa Sheria ya Maumbo Bunifu unalenga kuweka utaratibu au mfumo wa Kimataifa wa usajili na ulinzi wa Maumbo Bunifu kwa Nchi na Mashirika Wanachama wa WIPO ambapo mfumo huo utawezesha uwasilishaji wa maombi ya ulinzi wa Maumbo Bunifu kupitia WIPO ambapo mwombaji ataweza kuwasilisha ombi moja na kuchagua nchi zaidi ya moja ambazo zitakuwa zimeridhia Mkataba huo ambazo atahitaji kupata ulinzi wa ubunifu wake.
Wataalamu wa BRELA wamejiandaa kuwapitisha katika vifungu vya rasimu ya Mkataba wa Sheria hii ya kimataifa ya maumbo bunifu na mapendekezo yenu wadau yataboresha sheria hiyo ili itakapopitishwa na Nchi Wanachama iweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake. Maoni yenu pia yatatumika kutengeneza msimamo wa Nchi kuhusu kupitishwa kwa sheria hiyo, amesisitiza Bw. Nyaisa.

Ameendelea kusema kuwa, faida za mfumo huu ni kuongeza wigo wa ulinzi wa Maumbo Bunifu katika nchi nyingi kwa mara moja kupitia WIPO hivyo kupunguza gharama na ugumu wa ulinzi wa bunifu.
Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, endapo sheria hiyo itapitishwa na kuridhiwa kwa upande wa Tanzania, itatoa fursa na kuongeza wigo kwa wabunifu wa maumbo na michoro bunifu kusajili na kulinda bunifu zao katika ngazi ya kimataifa hivyo kukuza biashara na kuwawezesha kuhimili ushindani katika masoko ya ndani na nje.

Nae Bw. Mustafa A. Haji, Mrajisi Msaidizi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), akitoa salamu za Mkurugenzi Mtendaji, amesema kwa upande wa Zanzibar nyanja ya Miliki Ubunifu imekua kutokana na maboresho mbalimbali ya kisheria na kitaasisi ambayo yameboresha utoaji wa huduma za usimamizi wa miliki bunifu.
Dkt. Perfect Melkiory, Mhadhiri na Meneja wa Ofisi ya Usimamizi wa Miliki Ubunifu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kwa upande wao wamekuwa wakitoa elimu na usaidizi wa kuandaa maandiko ya bunifu zinazofanywa na wahadhiri pamoja na wanafunzi ili ziweze kulindwa

Ameendelea kusema kwamba, changamoto iliyopo kwa wabunifu wengi ni kutokuwa na mwamko wa kulinda bunifu zao mpaka pale wanapogundua bunifu zao zimeibiwa, na wengine wanarubuniwa kuuza bunifu zao kwa gharama nafuu kwa kampuni pasipo kujua umuhimu wa kitu alichokibuni.
Maumbo Bunifu ni moja ya nyenzo muhimu za Miliki Ubunifu inayohusiana na muonekano wa nje wa bidhaa au umbo la vifungashio/vibebeo vya bidhaa, mikebe, michoro, maumbo ya vito vya thamani, vifaa vya umeme, ubunifu wa mavazi na alama za picha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news