NA DIRAMAKINI
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana leo Septemba 1,2024 katika kikao chake maalum imewaondoa viongozi watatu wa chama hicho kwenye nafasi zao kwa kukiuka maadili ya uongozi.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Gabriel Makalla kupitia taarifa aliyoitoa leo ameeleza kuwa,walioondolewa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Jumuiya ya CCM Mkoa wa Lindi, Palina Ninje,
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani,Abdul Rashid Zahoro na Munira George Nkango ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Singida.
Katika hatua nyingine Kamati Kuu imefanya uteuzi wa majina ya Wana-CCM 10 kugombea nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kati ya Wanachama 47 walijitokeza kuwania uteuzi huo.
Walioteuliwa na Kamati Kuu ni Gladness Salema, Maria Alphonce, Queenelizabeth Makune, Ester Chaula, Prof. Neema Kumburu, Lucia Pande, Fatuma Kange, Hawa Mkwela, Fatma Msofe na Theresia Dominic.
“Wagombea walioteuliwa, watapigiwa kura kesho Jumatatu, Septemba 2, 2024 na kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, saa 8 mchana, Jijini Dodoma kisha Septemba 5, 2024 kutakuwa na uchaguzi wa kumpata Mbunge mmoja kwa kuchaguliwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao cha Kamati Kuu Maalum ya CCM, inayokutana jijini Dar Es Salaam, Jumapili Septemba 01, 2024.