DAR-Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba amewataka watumishi wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha wanatimiza majukumu kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi,kwani wakala huo ni taswira ya nchi katika sekta ya usafirishaji.

Pia, amewasihi kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo na sheria zilizopo,kwani watumiaji wa huduma za usafiri huo wa umma ni wananchi ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
“Wakala huu ni wakala muhimu sana na unabeba heshima kubwa sana ya nchi yetu kwa sababu tunajua Dar es Salaam ndio sura ya nchi na watu wote wakifika wanafikia Dar es Salaam.
"Kwa hiyo haya yaliyopo Dar es Salaam hasa huduma za msingi kama usafiri huu wa umma ndio yanajenga heshima ya nchi, hivyo tutimize majukumu yetu kwa viwango vinavyotakiwa,” amesema.