DC Gondwe aipongeza BoT kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu fedha na uchumi

SINGIDA-Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini, Mhe. Godwin Gondwe, Septemba 12,2024 ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya Saba ya Mifumo na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombadia mkoani Singida.
Akiwa katika banda la BoT, Mhe. Gondwe alielezea kufurahishwa kwake na kiwango cha weledi kilichoonyeshwa na wafanyakazi wa Benki Kuu katika kutoa elimu kwa wananchi.

Ameipongeza Benki Kuu kwa juhudi zake za kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya fedha.

"Nimefurahishwa na uwepo wa banda la Benki Kuu hapa Singida, na ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa kutuwezesha kupata fursa hii adhimu ya kufahamu fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hii muhimu," alisema.
Aidha, Mhe. Gondwe ameishauri BoT kuongeza juhudi za kusambaza elimu ya fedha kwa wananchi, hususan vijana.

Pia, alisisitiza umuhimu wa kutumia lugha nyepesi ili vijana wengi waweze kuelewa vizuri na kufaidika zaidi na fursa zinazopatikana.

“Nashauri muongeze bidii ya kueneza elimu ya fedha kwa vijana wengi zaidi, na ni vyema mkazingatia kutumia lugha zao ili muweze kwenda nao sambamba. Mkifanya hivyo, mtapata mafanikio makubwa katika kuwafikia," alisema.

Katika maonesho hayo, Benki Kuu ya Tanzania inatoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa mifuko ya udhamini wa mikopo kwa niaba ya Serikali. Mifuko hii ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo ya Mauzo Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS) na Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme - SME-CGS).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news