DCEA yamdaka Kinara wa dawa za kulevya Dar, tazama majina hapa

NA GODFREY NNKO

KINARA wa biashara za dawa za kulevya nchini, Richard Henry Mwanri mwenye umri wa miaka 47 akiwa na wenzake amekamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).

Ni kupitia operesheni iliyofanywa na DCEA kuanzia Agosti 28,2024 hadi Septemba 2,2024 katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 10,2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema, kupitia operesheni hiyo hiyo mamlaka imekamata kilo 1,815 za dawa za kulevya aina ya Skanka.

"Watuhumiwa waliokamatwa wanatambulika kwa majina ya Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Felista Henry Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguruni Mbezi, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya."

Kamishna Jenerali Lyimo amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Athumani Koja Mohamed (58) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Tanga.

Wengine ni Omary Chande Mohamed (32) ambaye ni dereva wa bajaji na mkazi wa Buza katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Vile vile yumo Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam. "Katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na Bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa."
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, Richard Henry Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuzisambaza nchini kwa usafiri wa magari.

Amesema, mtuhumiwa huyo huwa anazificha dawa hizo kwa kuchanganya na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini.

"Kwa siku za karibuni, dawa za kulevya aina ya Skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara nchini. Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambaye inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa ya maambukizi kama vile moyo, figo na ini,"amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news