PWANI-Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amewaeleza wananchi wake kuwa, atafanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha Wilaya ya Rufiji inaongoza kwa maendeleo nchini.
Mheshimiwa Mchengerwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Utete katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
"Kutoka kwenye nafsi yangu nitaendelea kuipigania Rufiji, niaendelea kufanya kazi kwa ajili yenu.
"Mimi ni mtumishi wenu nitaendelea kufanya kazi usiku na mchana, kila siku kuhakikisha tunabadilisha maisha yenu.
"Dhamira yangu ni kuibadilisha Rufiji, dhamira yangu ni kuona ndoto za waasisi wa wilaya hii ya Rufiji zimetimia.
"Wazee waliotangulia, wazee ambao walikuwa na ndoto kuona Rufiji imepiga hatua.Naomba niwathibitishie zile ndoto za waasisi na wazee wa wilaya hii nitahakikisha mchana na usiku zimetimia.
"Ninachowaomba kwenu ni dua, ndiyo jambo muhimu ninaloliomba kwenu. Dua ndiyo jambo kubwa ninaloliomba kwenu, lakini yapo mambo makubwa ambayo tunayaleta Rufiji ambayo hayakuwahi kutokea.
"Leo hii tumeendelea na maboresho makubwa katika hospitali yetu ya wilaya.Na ninyi mmejionea hali halisi ya hospitali hii,kule tulikokuwa mwaka 2015 na sasa tulipo mwaka 2024.
"Mabadiliko makubwa mmeyaona, lakini hivi karibuni Rais wetu nilimuomba fedha na ameridhia kuongeza fedha nyingine zaidi ya milioni 800 itaingia hivi karibuni ni lazima tuijenge hospitali hii ya wilaya kwa sababu ndiyo hospitali yetu kubwa.
"Hatuna hospitali nyingine kubwa isipokuwa hii ya Rufiji ambayo ipo hapa Utete, tutahakikisha vifaa vyote na vifaa tiba vinapatikana hapa.
"Na huduma zote zinapatikana hapa katika kipindi changu na kwa neema ya Mwenyenzi Mungu na dua zenu wana Rufiji mmejalia kwa dua zenu imempendeza Mheshimiwa Rais niwe Waziri wa TAMISEMI, baraka hizi ni za kwenu wana Rufiji, baraka hizi ni za kwenu wana Utete.
"Na mimi niwathibitishie sitawaangusha kamwe, nitakuwa wa mwisho kulala, nitakuwa wa mwisho kuisaliti Rufiji na haitatokea kamwe mimi kuisaliti Rufiji ninawathibitishia.
"Endeleeni kuwa na imani na mimi nitafanya kazi kubwa ya kujenga imani na kuingia kwenye mioyo yenu wa kwenda shule nitahakikisha anakwenda shule.
"Kila aliyemaliza shule nitahakikisha anapata mkopo wa elimu ya juu, yule anayetafuta kazi tutahakikisha tunamshika mkono ili kila mmoja wetu akaye katika mstari.
"Tulikuwa nyuma sana, tuna kazi ya kufanya ili kuhakikisha Rufiji hii kuwa zaidi ya popote pale hapa nchini.
"Niwahakikishie, imani mliyonayo kwangu ni deni ambalo ili nililipe lazima nifanye kazi kwa bidii kwa ajili ya kuleta maendeleo wialaya hii ya Rufiji.
"Niwathibitishie wazee ambao ninyi mlikaa na wazee waliotangulia mbele za haki yale ambayo waliwanong'oneza wakati mkiwa vijana nitapambana kuhakikisha tunayatekeleza.
"Zile barabara ambazo zinajengwa zitajengwa ile mitaa ya Utete ambayo haijakamilika lami nitapambana kuhakikisha inapitika lami, kama tunavyofanya maeneo mengine na hii ni ndoto ya Wanarufiji.
"Lini mliwahi kuota kuwa mtakuwa na lami Rufiji? Hayo yamewezekana kwa sababu mlinipa imani na mimi nikasema sitawaangusha kamwe na sitawaangusha hata kidogo,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Mchengerwa.