DODOMA-Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Divisheni ya Mikataba imeendesha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Mikataba. Mafunzo hayo ya siku tano yanawahusisha Mawakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mawakili wa Divisheni ya mikataba walioko Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka Mikoa mbalimbali nchini, Mafunzo tajwa yameanza leo tarehe 9 hadi 13 Septemba, 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kufungua Mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba, Bw. Sunday Hyera amesema lengo kubwa la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali juu ya Upekuzi wa Mikataba hususani Mikataba ya Ununuzi, pia Mawakili hao watapata kukumbushwa kuhusu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Divisheni hiyo kwa ujumla.
“Nawakaribisha sana kwenye mafunzo haya ambayo tunalenga kuwajengea uwezo Mawakili, mtapitishwa kwenye mada mbalimbali hususani Upekuzi wa Mikataba ya Ununuzi, tutafundishana kuhusiana na Mikataba ya Ununuzi na kupitia Sheria mpya ya Ununuzi ya Mwaka 2023 na Kanuni zake za Mwaka 2024, ili tuweze kutambua mambo gani tunatakiwa kuyafanya kwenye Mikataba ya Ununuzi”.
Vilevile Bw. Hyera amesema kuwa Mafunzo haya pamoja na kulenga Upekuzi wa Mikataba ya Ununuzi, pia yataambatana na mawasilisho ya mada mbalimbali kama vile Upekuzi wa Mikataba ya Fedha, Mikataba ya Maliasili, Mikataba ya Ushauri, na Mikataba ya Kimataifa na Makubaliano.
Pia ameelezea kuwa ana matumaini Mawakili hao watajifunza mambo mengi kwenye Mafunzo hayo na kwenda kusaidia kutekeleza wa majukumu yao kwa usahihi.
“Matarajio yetu baada ya Mafunzo haya Mawakili wetu watakuwa wamejifunza mambo mengi kuhusu mikataba hasa mikataba ya Ununuzi na kuyatumia mafunzo haya kuboresha utendajikazi wao.”
Akiwasilisha mada kuhusu Upekuzi wa Mikataba ya Ununuzi pamoja na Sheria mpya ya Ununuzi ya Mwaka 2023 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2024, Wakili wa Serikali Bw. Nyamhanga D. Nyamhanga amesema ni Mikataba yote ya Ununuzi yenye thamani zaidi ya bilioni moja inapaswa kuletwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya upekuzi, pia ameeleza kuwa hata Mikataba yenye thamani chini ya bilioni moja inaweza kuletwa kwa Mwanasheria Mkuu kwa upekuzi kwa hiari ya Taasisi zinazotaka kuingia Mkataba huo.
Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Bi. Shangwe Msungu amesema kuwa Mafunzo hayo yatawasaidia kupata uelewa wa pamoja juu ya masuala mbalimbali ya Mikataba na kuwasaidia katika kutekeleza kazi za
“Mafunzo haya yatatusaidia kuongeza uelewa juu ya mambo ya Mikataba, tutafahamu mchakato mzima wa namna ya kupekua Mikataba na Imani yangu kuwa baada ya mafunzo tutakwenda kuboresha utendaji kazi wetu.”
Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali wanaohusika na Mikataba ni mwendelezo wa jitihada za Divisheni ya Mikataba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajengea uwezo Mawakili hao ambapo Divisheni hiyo imejipanga kuendesha mafunzo kwa Mawakili kutoka Taasisi mbalimbali nchini.