Dkt.Biteko amwakilisha Rais Dkt.Samia mkutano wa Kimataifa wa Hydrogen nchini Namibia

WINDHOEK-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Hydrogen Barani Afrika unaoendelea nchini Namibia akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Mheshimiwa Dkt.Doto Biteko akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Netumbo Nandi-Ndaitwah jijini Windhoek leo.

Mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya Afrika, unajadili namna ya nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kutumia Hydrogen ambayo ni nishati safi na salama kwa mazingira na kwa uchumi endelevu.

Akifungua mkutano huo jijini Windhoek, Namibia, Makamu wa Rais wa Nchi hiyo, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewataka washiriki kutumia fursa ya mkutano huo kuainisha mbinu na mkakati unaoweza kutumika kuleta maendeleo ya nchi husika kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Akitoa mfano wa Namibia, Makamu wa Rais amesema Namibia inajivunia matumizi ya Hydrogen kwa matumizi ya viwanda kwa manufaa nchi hiyo, nchi Jirani pamoja na mataifa mengine yaliyo katika mlengo wa matumizi ya nishati hiyo.

Aidha, amehimiza matumizi ya nishati safi kwa maendeleo ya nchi hizo huku akisisitiza ushirikishaji wa vijana kama nguzo muhimu ya maendeleo kwa bara la Afrika kutokana na mchango na uwezo wao kama nyenzo ya maendeleo katika nchi husika.

“Majadiliano haya ni muhimu yakazingatia ushirikishaji wa pande zote muhimu katika mkutano huu wa kimataifa ili kuwa na maendeleo ya kweli na endelevu kwa uchumi na maendeleo ya watu na nchi zao,”amesema Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Awali katika majadiliano, Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mhe. Tom Alweendo amesema wajumbe wa mkutano wanatakiwa kuzingatia kuwa nchi za Afrika na Washirika wake zinatakiwa kuzingatia kuwa matumizi ya rasilimali zilizopo yanahitaji ushirikiano badala ya ushindani.
Amesema, Namibia imekuwa ikishirikiana na nchi nyingine barani Afrika katika matumizi rasilimali zilizopo na nchi nyingine washiriki zinakaribishwa kuunga mkono jitihada hizo ikiwemo uzalishaji na matumizi ya Hydrogen kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi ya kupikia na kuendesha shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Mhe. Tinne Van Der Straeten amewataka washiriki kuhimiza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa njia mojawapo ya kuwakomboa watu wa nchi hizo dhidi ya umasikini.
Amesema, matumizi ya nishati mbadala ikiwemo Hydrogen ni moja mkakati madhubuti wa kuwakwamua watu na nchi zao katika lindi la umaskini na kuwawezesha kushiriki katika mipango mingine ya maendeleo.

Tanzania kwa upande wake, imetumia fursa ya mkutano huo kujifunza kuhusu faida na changamoto zinazoweza kujitokeza katika matumizi ya nishati safi inayotokana na Hydrogen ikiwa ni pamoja na uzoefu kutoka nchi nyingine zinazotumia nishati hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameungana na Makamu wa Rais wa Namibia Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwa kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho kuhusu matumizi ya Hydrogen yanayokwenda sambamba na Mkutano huo.

Baada ya maonesho hayo, Naibu Waziri Mkuu alikutana na Makamu wa Rais wa Namibia kwa mazungumzo ya ndani yaliyolenga kujadili masuala mbalimbali yahusuyo ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Katika Mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amefuatana Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Cesar Waitara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news