Dkt.Biteko ashiriki dua ya Mzee Majid Nsekela, atoa wito kwa jamii

KAGERA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameiasa jamii kuwa na utaratibu wa kuwatunza na kuwajali wazazi wao na kuendelea kuwaombea ambao hawapo hai.
“Tuendelee kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na wazazi waliotangulia mbele za haki ni jambo zuri na wajibu wetu tuliobaki, Sheikh wetu katika mawaidha yake ameliongelea kwa uzuri sana.

"Tulitilie maanani na sote tuendelelee kufanya hivi, na kama huwa hatuwafanyii hivi ndugu zetu, hatuna budi tuanze kwa moyo wote.”
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Septenba 7, 2024 akiwa Nyakatuntu, Kyerwa mkoani Kagera wakati aliposhiriki katika dua ya kuwaombea baba mzazi na ndugu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Mussa Nsekela

"Ndugu zangu tusisahau mapito yetu. Katika mapito huwa kuna watu. Katika watu hawa, kuna wazazi wetu.

"Kama wazazi wako wapo hai, mmoja au wote au wale waliokulea, jua nawe una wajibu wa kuwalea na kuwatunza, siyo kifedha tu bali pia kwa mahusiano mema hasa ya kihisia kwa kuwa hivyo ndivyo impendezavyo Mungu.
“Mzee wetu, Rais wa Awamu ya Pili, Marehemu Ally Hassan Mwinyi, Mzee Rukhsa alituasa kuwa maisha yetu hapa duniani si kitu ila ni hadithi tu na kuwa tuyafanye maisha yetu yawe hadithi nzuri. Kwa dua hii, kwa umati huu.

"Kwa wanafamilia hawa wa Nsekela inadhihirisha bayana kabisa kuwa maisha ya Mzee wetu, Alhaji Tibihika Mussa Nsekela, na wengine tuliowaombea dua leo hapa yameacha hadithi nzuri kwa sisi tuliobaki hili ni jambo zuri la kujifunza.”
Aidha, Dkt. Biteko ameendelea kuiasa jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao wanapotoka, kuendelea kuishi kwa upendo sambamba na kuishukuru familia hiyo kwa kumualika kushiriki katika dua hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea na jitihada zake mbalimbali za kuwaletea maendeleo wananchi wa Nyakatuntu kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya ya Kyerwa na tayari imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi wa barabara.
Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuber amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baba yake na kusema kwa kufanya hivyo inaonesha anaipenda familia yake nq dini yake ya kiislamu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Majid Nsekela amesema kuwa tukio hilo kwao ni la historia na wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo.
"Kwa dua hii ya leo tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na kuwa na kazi nyingi amejumuika nasi hapa na wote mliopo nasi leo kwa upendo wenu na familia yote imefurahi na inawashukuru,” amesema Bw. Nsekela.

Aidha, Bw. Majid amewakumbusha na kuwatakia heri wananchi wa Nyakatuntu kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu kwa kuchagua viongozi wanaofaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news