DODOMA-Benki ya Exim ya nchini Korea Kusini imeonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini Tanzania kutokana na uwepo wa fursa nyingi za uwekezaji hususan katika miradi ya kimkakati inayoratibiwa na serikali kupitia Wizara ya Madini.

Akizungumza katika kikao Kyeong amesema kuwa, ushirikiano wa Benki ya Exim ya Korea Kusini na sekta ya madini Tanzania utasaidia kuongeza ufanisi , ajira na mapato katika mnyororo mzima wa thamani madini na kuendelea kuimarisha Tanzania kama kitovu cha madini barani Afrika.
Kyeong ameongeza kuwa, kuwepo kwa ushirikiano huo kutafungua milango ya uwekezaji kwa kampuni za Korea Kusini katika kuchangia hususani katika matumizi ya tekinolojia kwenye utafiti na uchimbaji pamoja na kuongeza mzunguko wa rasilimali fedha katika mnyororo mzima wa madini.
Kwa upande wake , Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo amesema kuwa, sekta ya madini nchini Tanzania inaendelea kukua kwa kasi na kuendelea kutanua wigo wa mashirikiano ya kisekta hususan katika kuibua miradi ya kimkakati kwenye madini mkakati na adimu.
Mbibo amefafanua kuwa, pamoja na mambo mengine Tanzania kwa kipindi kirefu imekuwa na mashirikiano ya kimkakati na Korea Kusini kupitia Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali madini (KIGAM) katika kuendeleza na kuibua fursa mpya katika sekta ya madini.

Katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu aliambatana na wataalam wengine wa wizara ya madini.