MWANZA-Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imeendesha mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu ugonjwa wa sikoseli kwa wataalamu wa afya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Mafunzo hayo yametolewa na Madaktari Bingwa wa Sikoseli na magonjwa ya damu sambamba na Mtaalamu wa Maabara Kitengo cha Damu ambao ni Dkt. Emmanuela Ambrose, Dkt. Tekla Mtobesya na Mwesige Charles.
Aidha,mafunzo haya yamehusisha wataalamu wa 63 wakiwemo Madaktari, Wauguzi, Wahudumu wa Afya na wataalamu wengine na yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 11-13 Septemba 2024 wilayani Sengerema.
Ni kufuatia maombi ya Halmashauri ya Sengerema kuhitaji wataalamu wake kupewa mafunzo na kuanzisha clinic za Sikoseli ikiwa ni huduma ya uchunguzi wa awali kwa wagonjwa wa sikoseli kabla ya kupewa Rufaa.
Kupitia mafunzo haya, washiriki wameweza kufundishwa jinsi ya kugundua ugonjwa kitaalamu, namna ya kumuhudumia mgonjwa na kutoa rufaa mapema inapohitajika.
Septemba ni mwezi wa uhamasishaji wa Ugonjwa wa Sikoseli ambao unalenga kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huu na changamoto wanazokabiliana nazo watu wanaoishi na hali hii duniani kote.