Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma afanya ukaguzi

NA KANDANA LUCAS
Mahakama Musoma

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya amefanya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za Mwanzo zilizoko ndani ya Kanda hiyo, ikiwa ni ukaguzi wa kawaida wa robo ya tatu ya mwaka 2024.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya(aliyenyoosha mkono), viongozi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Wilaya Bunda wakikagua mipaka ya eneo la Mahakama ya Mwanzo Mugeta-Bunda.

Katika ziara hiyo ya ukaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, Mhe. Jaji Mfawidhi aliwapongeza watumishi wote wa Mahakama zilizokaguliwa kwani wamefanikiwa kutekeleza kwa weledi majukumu yao na maelekezo mbalimbali ya viongozi wakuu wa Mahakama ya Tanzania ngazi ya Makao Makuu na Kanda.

Mhe. Jaji Mtulya alibainisha baadhi ya maelekezo ambayo kwa nyakati tofauti yamekuwa yakisisitizwa na viongozi na yamefanyiwa kazi ni pamoja na kuweka kipaumbele cha usikilizwaji wa mashauri ya mlundikano, matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kusikiliza kwa wakati mashauri ya mirathi, ndoa na talaka.
Jaji Mfawidhi akisisitiza jambo kuhusu uwekaji wa alama katika mipaka ya maeneo ya Mahakama, alipokagua eneo la Mahakama ya Mwanzo Mcharo.

Aliyataja maelekezo mengine kuamua kwa wakati mashauri yanayohusu taasisi za kifedha (mabenki), kushughulikia mashauri yanayohusu ukatili wa kijinsia, utekelezaji /ukazaji wa hukumu pamoja na masharti nafuu ya dhamana katika Mahakama za Mwanzo ili kuepuka mlundikano wa mahabusu magerezani.

“Ninapenda kutoa pongezi kwa viongozi na watumishi wote wa Mahakama nilizozikagua, kwani kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kutekeleza maelekezo ya viongozi na mikakati mbalimbali ambayo ilitokana na kaguzi zilizopita pamoja na vikao vya Menejimenti Kanda...
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Butiama Mhe. Judith Semkiwa akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo katika ukaguzi huo.

“Kwa kufanya hivyo, wameweza kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama kwa vitendo hasa Nguzo ya Tatu inayohusu kurejesha Imani kwa Wananchi na Ushirikishaji Wadau. Aidha nawahimiza Wahe. Mahakimu kuendelea kuyapa kipaumbele mashauri ya kimkakati yanayohusu mirathi, ndoa na talaka, mashauri ya madai yanayohusisha taasisi za kifedha pamoja na mashauri ya mlundikano ili kama Kanda tusivuke na mashauri ya muda mrefu ifikapo tarehe 31 Desemba,2024,” Mhe. Jaji Mtulya alisema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Fahamu Hamidu Mtulya (katikati) viongozi wa Mahakama Kuu Musoma, wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Butiama na Mahakama ya Mwanzo Kiagata iliyopo Wilaya ya Butiama baada ya kufanya ukaguzi.

Vilevile Mhe. Jaji alitoa wito kwa viongozi wa Mahakama ndani ya Kanda kuhusu kuweka mpango endelevu wa upandaji miti, upimaji wa maeneo ya Mahakama, kuweka alama tambuzi (bikoni) na kufuatilia upatikanaji wa hati za viwanja ili kulinda mipaka ya maeneo ya Mahakama hasa Mahakama za Mwanzo kwani kutofanya hivyo maeneo mengi ya Mahakama yanaweza kuvamiwa na wananchi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya(katikati), viongozi wa Mahakama Kuu Musoma wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Butiama.

Viongozi wengine waliombatana na Mhe. Jaji Mtulya katika ukaguzi huo ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora, Mtendaji wa Mahakama wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma,Bw.Leonard Maufi na Afisa Tawala Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bw. Kandana Lucas ambao kwa upande wao walipongeza kuhusu namna maelekezo mbalimbali yalivyotekelezwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya(katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama Kuu, viongozi wa Mahakama ya Wilaya Tarime na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Mtana-Tarime baada ya ukaguzi wa mipaka ya eneo la Mahakama hiyo.

Huku viongozi wa Mahakama walioambatana naye waliahidi kuyafanyia kazi masuala ambayo yaliibuliwa na Mahakama zilizokaguliwa yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi wa Mahakama Kuu au Makao Makuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Hamidu Mtulya, akiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tarime baada ya ukaguzi wa Mahakama hiyo.

Jumla ya Mahakama zilizokaguliwa na viongozi hao ni 14 ambazo ni Mahakama ya Mwanzo Kiagata-Butiama, Mahakama ya Wilaya Butiama, Mahakama ya Wilaya Bunda, Mahakama ya Mwanzo Bunda Mjini, Mahakama ya Mwanzo Mcharo-Bunda, Mahakama ya Mwanzo Mugeta-Bunda, Mahakama ya Mwanzo Natta-Serengeti, Mahakama ya Wilaya Serengeti, Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Mugumu Mjini, Mahakama ya Wilaya Tarime, Mahakama ya Mwanzo Mtana-Tarime, Mahakama ya Wilaya Rorya, Mahakama za Mwanzo Ingri na Nyaburongo zote za Wilaya ya Rorya pamoja na Gereza la Wilaya Musoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news