NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Kampala
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 30 Septemba, 2024 amewasili nchini Uganda kuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akizungumza na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Divisheni ya Biashara, Mhe. Suzan Abinyo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Entebe leo tarehe 30 Septemba, 2024 kuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Mhe. Prof. Juma na ujumbe wake amewasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Entebe majira ya saa 6.00mchana na kupokelewa na Jaji wa Mahakama Kuu Uganda, Divisheni ya Biashara, Mhe. Suzan Abinyo na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Maj. Gen. Paul Kisesa Simuli.
Katika mkutano huo, Jaji Mkuu ameongozana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Leila Edith Mgonya na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kamazima Kafanabo Idd, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Mkuu wa Itifaki Juma Mshana Kapombe na watumishi wengine wawili wa Mahakama.
Ujumbe huo wa Mahakama ya Tanzania unahudhuria Mkutano huo utakaofanyika kuanzia kesho tarehe 1 Oktoba, 2024 katika hoteli ya Munyonyo jijini hapa. Mkutano huo umeandaliwa na Mahakama ya Uganda kwa kushirikiana na kamati maalum kutoka SEACJF.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Katika Mkutano huo kutakuwepo na mjadala mpana kuzungumzia dhana ya maboresho katika Mahakama barani Afrika ili kuimarisha upatikanaji wa haki atuzi wa migogoro barani Afrika.
Mkutano huo unawaleta pamoja Majaji Wakuu kutoka nchi mbalimbali Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika na Watalaam ili kutoa fursa kwa Mahakama na watendaji wengine wa haki kujadili kwa kina namna maboresho katika Mahakama yanavosaidia kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Maj. Gen. Paul Kisesa Simuli baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Entebe.
Wanasheria mashuhuri na wataalam wa sheria kutoka katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo watashiriki katika mijadala ya kina wakati wa mkutano huo.