Wafanyabiashara waliouawa Songea wazikwa kimya kimya porini, wafukuliwa

DODOMA-Jeshi la Polisi linawashikilia Mtila Ausi maarufu Shehe Mtila ambaye ni mganga wa kienyeji, Omary Abdallah na Amini Sanga kufuatia vifo vya wafanyabiashara wawili mkoani Ruvuma ambao ni Raymond Hyera na Riziki Mohamed waliofika kwa mganga huyo.

Lengo ni kupata dawa za kuwawezesha biashara zao kufanya vizuri zaidi na wakapewa maji yaliyowafanya walegee na kufariki na kisha wakazikwa kimyakimya.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime kupitia taarifa aliyoitoa Septemba 04,2024 amefafanua kuwa, “Agosti 3, 2024 katika Kituo cha Polisi Songea Mkoa wa Ruvuma, zilipokelewa taarifa za kupotea kwa wanyabiashara wawili toka Julai 31, 2024.

"Wafanyabiashara hao walitajwa na ndugu waliofika kituoni kutoa taarifa kuwa ni Raymond Hyera jina maarufu Ray (25) mkazi wa eneo la Msamala, Manispaa ya Songea na Riziki Mohamed (30) mkazi wa eneo la Mjimwema, Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma.

“Baada ya uchunguzi na mahojiano, mganga na wenzake walikiri wafanyabiashara hao kufika nyumbani kwao wakiambatana na mfanyabiashara mwenzao aitwaye Amini Sanga kwa lengo la kupata dawa za kuwawezesha biashara zao kufanya vizuri zaidi.

"Waliwanywesha maji ambayo yaliwafanya walegee na kupelekea kupoteza maisha, baada ya kufariki, waliwachukua na kwenda kuwazika katika pori la Mdinguli, Kijji cha Mtangashari, Tunduru kisha kuchukua fedha walizokuwa nazo shilingi milioni ishirini na kugawana.

“Septemba 3, 2024, Mtila Ausi na Omary Abdallah waliwaongoza Polisi hadi walipowazika wafanyabiashara hao, ufukuaji ulifanyika na miili ya wafanyabiashara hao ilikutwa, uchunguzi unaendelea kukamilishwa ukiwepo wa kisayansi ili taratibu nyingine zifuate;

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news