Jipangeni utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote-Katibu Mkuu

ARUSHA-Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kujipanga na kuweka mikakati ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ili kufanikisha matarajio ya ya Serikali na wananchi.Hayo ameyasema leo jijini Arusha wakati akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la NHIF waliokutana kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma kwa wadau wake.

“Jambo la Bima ya Afya ni kubwa, lazima tujipange vizuri katika utekelezaji wake, Sheria na Kanuni zimeshasainiwa na katika hili niwahakikishie Serikali iko na ninyi katika kila hatua ili muweze kufanikisha hili,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Amesema kuwa, ili kufanikisha suala hilo, Mfuko ujikite katika matumizi ya Mifumo na kuongeza ubunifu katika vitita vyake ili kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake.
Akizungumzia utendaji kazi, amewakata Watumishi kuwajibika katika maeneo yao kwa kutambua dhamana kubwa iliyowekwa na Serikali kwa Mfuko kuhudumia wananchi wake.

“NHIF mna dhamana kubwa sana na ni nguzo kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu nchini, hakikisheni mnaboresha utendaji kazi wenu ili huduma mnazozitoa ziweze kwenda na wakati au mahitaji ya sasa,” amesema Katibu Mkuu.
Aidha, ametumia fursa hiyo, kuonya baadhi ya wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu na kuwataka kuacha mara moja na badala yake kuwa walinzi wa huduma ili Mfuko uendelee kuwa hai na kutoa huduma bora.

Katibu Mkuu amempongeza Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Irene Isaka kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuiongoza NHIF ambayo ni taasisi nyeti na nguzo katika sekta ya afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Irene Isaka, amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa watumishi wote wa Mfuko wako tayari kutekeleza suala la Bima ya Afya kwa wote ili matarajio ya Serikali na wananchi yaweze kufikiwa.“Tutafanya kazi kwa nguvu zote na weledi mkubwa, tumejipanga na tunafanya kazi kubwa kuweka mifumo yetu vizuri ili iweze kurahisisha utoaji wa huduma zetu,” alisema Dkt. Isaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news