Kamati yapendekeza kufutwa kwa viwanja saba Mtwara Mikindani

MTWARA-Kamati ya Mipango Miji Manispaa ya Mtwara-Mikindani imetembelea viwanja saba vilivyopo maeneo ya mjini katika Kata ya Shangani, Chuno na Magomeni na kupendekeza kufutwa kwa miliki za viwanja hivyo ambavyo vimemilikishwa kwa muda mrefu na havijaendelezwa.
Viwanja hivyo vimemilikishwa zaidi ya miaka 20 na kutokuendelezwa kabisa kinyume na masharti ya umiliki na uendelezaji ardhi yaliyoainishwa katika hatimiliki za viwanja husika.

Kamati hiyo imejiridhisha na mapendekezo ya ufutaji wa miliki za viwanja husika na hivyo kuelekeza kuwa taratibu zote za kisheria zifuatwe na mapendekezo ya ufutaji au ubatilishaji wa miliki hizo yawasilishwe kwenye ngazi zinazohusika.

Ni ili taratibu za ufutaji wa miliki hizo zitakapokamilika, viwanja hivyo viweze kugawiwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji na uwezo wa kuendeleza kwa wakati.

Mkuu Idara ya Mipango Miji,Maiga Rugembe amesema kuwa,zoezi la ukaguzi wa viwanja visivyoendelezwa pamoja na kuchukua hatua za kubatilisha au kufuta miliki za viwanja visivyoendelezwa ni endelevu na litaendelea kufanyika kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ardhi sura 113 na Kanuni zake za mwaka 2001.

Ametoa rai kwa wananchi wote wanaomiliki viwanja katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kutekeleza masharti ya umiliki yaliyoainishwa kwenye nyaraka zao za umiliki (hatimiliki).

Amekumbusha masharti hayo kuwa ni pamoja na kulipia kodi ya pango la ardhi kwa kila mwaka, kuendeleza viwanja ndani ya kipindi cha miezi 36 tangu walipomilikishwa kwa kupewa kibali cha ujenzi kutoka halmashauri husika.

Pia,kulinda na kutunza alama za mipaka ya kiwanja pamoja na kulinda na kutunza kiwanja au viwanja dhidi ya uvamizi au uharibifu wowote.

Ameendelea kusisitiza kuwa,kushindwa kutekeleza masharti hayo ni kukiuka masharti ya umiliki na hivyo kupelekea kufutiwa umiliki na kiwanja au viwanja husika.

Vilevile amewataka wamiliki wa viwanja kurekebisha kasoro au dosari hizo za umiliki kwa kuzingatia na kutekeleza masharti ya umiliki ili kuepuka kufutiwa haki ya umiliki wa viwanja vyao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news