Kamati yataka kasi ujenzi makao makuu Wizara ya Madini

DODOMA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imemtaka Mkandarasi wa Jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Madini linalojengwa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kasi ili kukamilisha Mradi huo kwa ubora na muda uliopangwa bila kuchelewa.
Agizo hilo limetolewa Septemba 4, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Mathayo David wakati wa ziara ya Kamati hiyo kukagua maendeleo ya mradi huo.

Ameeleza kuwa, kuchelewa kukamilika kwa jengo hilo kunaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa Wizara ya Madini, ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa sekta ya madini nchini.
“Wote tunafahamu kuwa Wizara ya Madini ni nguzo kuu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika pato la taifa, Mkandarasi sisi kama Bunge tunachotaka kuona ni nyie kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huu na kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kuipa wizara uwezo wa kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa kukamilika kwa jengo la Makao Makuu hayo ya Wizara kutatusaidia kufanya shughuli za usimamizi wa Sekta ya Madini kwa ufanisi mkubwa kutoka katika eneo moja.

“Sisi kama Wizara tunashukuru kwa ziara yenu hii Kamati ya Bunge, tunaamini itasaidia kuongezeka kwa kasi katika ukamilishaji wa mradi, lengo la Wizara ni kufanya shughuli zote katika eneo hili kwa watendaji na wafanyakazi wetu kukaa hapa (one stop center),” amesema Dkt. Kiruswa.
Naye, Mhandisi wa Mradi huo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mhandisi Remigius Kaijage amesema kuwa ujenzi wa mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 23 umefikia asilimia 85 na tayari vifaa vyote vipo eneo la kazi na kwamba kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kutoka kwa Mshauri ambao ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mradi huo utakamilishwa kwa ubora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news