PWANI-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni, na Michezo imetembelea Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya elimu na kutathmini utekelezaji wake. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, ameipongeza serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua nzuri za utekelezaji wa miradi hiyo, akibainisha kuwa inaridhisha kwa kiasi kikubwa.
Kamati hiyo ilitembelea miradi miwili, ambayo ni Shule ya Sekondari ya Shimbo pamoja na Shule ya Elimu ya Watu Wazima, zilizopo Halmashauri ya Kibaha. Miradi yote iko katika hatua za mwisho za kukamilika, huku wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Shimbo wakiwa tayari wameshaanza masomo.
Baada ya ukaguzi, kamati kupitia kwa Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Husna Juma, ilisisitiza umuhimu wa viwango vya ujenzi wa miradi hiyo kuwa sambamba na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali.
Pia, ilipendekeza miradi ya halmashauri kuwa na viwango sawa na ile ya Serikali Kuu, huku ikiwezekana kusisitizwa kubadilishana uzoefu kati ya wasimamizi wa miradi hiyo.
Kamati pia ilishauri serikali kuhakikisha fedha za miradi zinapelekwa kulingana na mahitaji ya maeneo husika ili kuepusha matumizi yasiyo sahihi. Mheshimiwa Husna alitoa mfano wa tofauti ya bei ya saruji kati ya mikoa ya Kigoma na Tanga, akibainisha kuwa hali hiyo inaweza kusaidia kupunguza matumizi mabaya ya fedha za miradi.
Aidha, kamati imeitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha vitabu vyote vinavyosambazwa mashuleni vinapitiwa na kugongwa mhuri na Kamishna wa Elimu ili kuhakikisha vinaendana na maadili ya Kitanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Adolf Mkenda, aliiagiza Halmashauri ya Kibaha kufuatilia suala la kukamilisha uzio wa shule, ambalo bado halijatekelezwa kikamilifu. Kuhusu suala la vitabu, Mheshimiwa Mkenda alisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa uandishi wa vitabu vya kiada ili kuendeleza na kulinda maadili ya Kitanzania.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng'umbi, alipendekeza kuanzishwa kwa kada maalum ya Elimu ya Watu Wazima katika vyuo vikuu ili kupata wataalamu waliobobea katika ufundishaji wa elimu hiyo.