Kamishna Jenerali Lyimo aongea na wasanii kwa upole, aahidi ushirikiano lakini dawa za kulevya hapana

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imeahidi kuendelea kushirikiana na wasanii mbalimbali nchini katika kuhakikisha kazi zao za sanaa zinakuwa na matokeo chanya kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo (katikati) akiwasili katika Tamasha la Faraja ya Tasnia lililofanyika Septemba 7,2024 viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Pia, DCEA imewataka wasanii kote nchini kutumia karama na vipaji vyao kuandaa kazi za sanaa ambazo ndani yake zitakuwa na vionjo vya kukemea matumizi na biashara ya dawa zz kulevya nchini.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ameyasema hayo Septemba 7,2024 katika Tamasha la Faraja ya Tasnia lililofanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo ametambua umuhimu wa wasanii katika jamii na kuwataka waendelee kutumia vipaji vyao katika kupambana na dawa za kulevya huku akitoa bima kwa familia 10 za wasanii wa Tanzania waliofariki dunia.
"Ni jambo jema sana ambalo tunatakiwa tuliendeleze na Watanzania wote tuunge mkono wasanii ili kuhakikisha kwamba tunajenga Taifa moja, Taifa lenye upendo, Taifa lenye muunganiko.

"Lakini pia kumsapoti Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kulileta taifa katika umoja wake ili tuwe na kitu kimoja katika taifa moja kuweza kulinda amani yetu, uchumi wetu pamoja na uhuru wetu.

"Mimi,Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ninawapongeza sana kuhusu hilo, lakini pia ninaungana na ninyi katika kuhakikisha kwamba tunaendeleza sanaa yetu, tunaungana pia na Mheshimiwa Rais ambaye ameona thamani kubwa mliyonayo ninyi wasanii na kuamua kuwaleta pamoja.

"Ni katika kuhakikisha kwamba tunajenga Taifa moja lenye amani na upendo, lakini pia tukitimiza zile 4R zake za kuhakikisha kwamba ili Taifa linasonga mbele."

Falsafa ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan zimejikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

"Kwanza kabisa wasanii ni watu muhimu sana katika jamii, wasanii ni tiba, wasanii ni dawa kwa sababu hata mtu akitaka kujinyonga akisikiliza au akiona kazi za wasanii anahairisha kujinyonga akiona kwamba dunia ni njema, dunia ni nzuri kwa nini nijinyonge, kwa nini nijiue.
"Wasanii wanaondoa matatizo, wasanii wanaondoa misongo ya mawazo, wasanii wanaleta faraja katika jamii.

"Kwa hiyo sisi mamlaka (DCEA) pia na sisi tunaopambana na dawa za kulevya tunawaomba pia wasanii katika nyimbo zenu katika tasnia hii ya usanii tuhakikishe kwamba tunafikisha ujumbe kwa jamii.

"Ili kuhakikisha kwamba pia tunaokoa vizazi vyetu dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya ili tuweze kulinda afya za wananchi, afya zetu kama wasanii,lakini afya za jamii kwa ujumla.

"Na hili taifa liweze kuwa na afya na taifa liweze kusonga mbele, lakini pia katika kutimiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha kwamba inajenga uchumi endelevu na katika kujenga uchumi endelevu, afya za wananchi ni muhimu sana.

"Mheshimiwa Rais akiwa Kamanda Mkuu wa kulinda afya zetu na katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya tuendelelee kumuheshimisha kwa kuhakikisha kwamba tunapambana na dawa za kulevya kama wasanii na kwenye kazi zetu za kisanii tuweke vionjo ambavyo vinaonesha na kupeleka elimu kwa jamii kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya ili wananchi waliowengi ikiwemo sisi wenyewe tuendelelee kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya.

"Lakini, mimi mara nyingi huwa ninawapenda sana wasanii na huwa ninapenda kuangalia sana nyimbo au kazi za wasanii kwa sababu ninaamini ninapata tiba kule, kwa sababu ninapata faraja ya moyo kulingana na kazi zile mnazozifanya.

"Lakini,kuangalia huko si kufuatilia ni nani pengine anahamasisha dawa za kulevya ili tuweze kumfuatilia hapana. Ni kupata pia faraja kama Mtanzania na kuzithamini kazi zenu.

"Sasa hivi kwa kuwa ni mara ya kwanza kusimama mbele yenu kama kijana tunaoshirikiana katika masuala haya ya kisanii, sasa ninaomba pia mnilete katika familia ya kisanii ili tuweze kushirikiana kwa pamoja.

"Tuweze kushirikishana kazi mbalimbali za kisanii na shughuli mbalimbali za kisanii na mamlaka (DCEA) iko tayari kuungana na ninyi, kushirikiana na ninyi katika kazi zenu za kisanii ili kuhakikisha kwamba, tasnia ya kisanii kwa kuwa ni kioo cha jamii nasi tunaendelea kuilinda.

"Tunaendelea kuhakikisha kwamba inakuwa na kuhakikisha inaleta faraja kwa Watanzania na tasnia hii ya usanii iweze kuonekana ndiyo kazi muhimu katika jamii.

"Kwa sababu, tasnia ya usanii ni kioo cha jamii na kioo cha jamii ndicho kinachoonesha jamii ikoje katika maadili na katika kulinda uhuru na uchumi wetu.

"Na kwa kuwa, wasanii ni kioo cha jamii tunaithamini sana na tunaomba sasa tuwe pia tunawatumia wasanii katika kuhakikisha kwamba tunafikisha jumbe mbalimbali kwa wananchi ili kuhakikisha kwamba na wao wanajilinda dhidi ya dawa za kulevya.

"Lakini, pia maadili ya nchi na kuhakikisha kwamba tunaendeleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tuna taifa moja, taifa lenye amani, taifa lenye upendo na taifa linalokuwa kiuchumi.

"Lakini pia, taifa ambalo linaunganisha watu wote na kuwa watu wamoja na tunapokuwa watu wamoja ina maana hakuna adui yeyote anayeweza akaingia ndani yetu na kuweza kututenganisha.

"Kwa hiyo Watanzania wote niwaombe pia kupitia tukio hili tuwaunge wasanii mkono kuhakikisha kwamba tunashirikiana nao kwa pamoja kama tasnia muhimu sana katika jamii zetu katika kuliunganisha taifa, lakini katika kutoa burudani kwa taifa lakini kuleta faraja ya moyo katika taifa letu.

"Lakini, pia katika kuungana na Mheshimiwa Rais, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itatoa vifurushi 10 kwa familia 10 za wale ambao wametangulia mbele ya haki.
"Tutawakatia bima za afya kwa familia 10 ili tuweze kuungana na Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha tunawafariji hawa ambao wametangulia mbele za haki.

"Lakini, kuonesha kwamba tunathamini kazi zao ambazo wamezifanya wakiwa hapa duniani na kuthamini yale ambayo wametufundisha, yale mema waliyotuachia na kuthamini zile kazi zao.

"Lakini, pia na sisi ambao tupo duniani tuendelelee kuhakikisha kwamba tunafanya kazi za kisanii ambazo zinaleta tija, zinaleta faraja, tunalinda brand zetu na kuhakikisha kwamba tunaifundisha jamii.

"Tunaiburudisha jamii na kuleta yale ambayo ni miongoni mwa yale yanayoijenga jamii, Serikali, yanayoijenga nchi, yanayojenga Taifa na kuleta amani, furaha na upendo wa Watanzania,"amefafanua kwa kina Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news