NA DIRAMAKINI
TANZANIA inatarajia kuandaa Kongamano la Kihistoria la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambalo litazikutanisha nchi mbalimbali barani Afrika.
Hayo yamebainishwa Septemba 10,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini (ICTC),Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga katika kipindi cha Twende Pamoja cha Channel 10 jijini Dar es Salaam.
"Ili kongamano ni la kihistoria kwa sababu katika Bara la Afrika kwa mara ya kwanza kuna Shindano la Akili Mnemba na Roboti kwa vijana wote wa Afrika ambalo litazinduliwa kwa mara ya kwanza Tanzania.
"Na hili limeenda sambamba na kongamano letu la TEHAMA la Taifa ambalo kwa mwaka huu kauli mbiu yake inasema kutumia Akili Mnemba na Roboti katika Kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi na Kijamii.
"Kwa hiyo, hii tumeiangalia kwa ujumla wake kuangalia hii Akili Mnemba inaweza ikatumika vipi."
Dkt.Mwasaga amesema, kongamano hilo linafanyika mwezi Oktoba kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 17,2024.
"Na kongamano hili litakuwa la siku tano, kutakuwa kuna mambo mengi sana pale yanayohusiana na hiyo kauli mbiu na vile vile maonesho mbalimbali ya kampuni changa za startups za ndani ya nchi na nje ya nchi.
"Na mada mbalimbali zitakuwa zinajadiliwa pale na kuweza kuona sasa hayo mashindano ya Afrika ya Vijana katika eneo la Roboti na Akili Mnemba itakavyokuwa, washindi ni kina nani na kina nani walishindanishwa."
Amesema, katika mashindano hayo ziliingia bunifu 1,008 za vijana kutoka Afrika nzima.
"Kwa hiyo hizo tunazichakata halafu watapatikana washindi katika maeneo mbalimbali."
Amesema, mashindano hayo yatafanyika kila mwaka kuwashindanisha vijana wa Afrika ili kukuza ubunifu katika maeneo ya Akili Mnemba na Roboti.
Mchango wa TEHAMA
Dkt.Mwasaga akizungumzia mchango wa TEHAMA katika maendeleo ya Taifa amesema, "Sekta ya TEHAMA ukiangalia ni sekta mtambuka na inatumika katika sehemu nyingi, katika sekta mbalimbali.
"Ukiangalia sasa hivi kwa mfano katika Sekta ya Elimu tukianzia unakuta kuna namna mbalimbali watu wanaweza kupata zile taarifa au masomo ya elimu kwa kutumia mtandao vizuri.
"Sehemu yote ambayo tunapeleka mawasiliano,ninadhani umeona, Serikali imefanya jitahada kubwa za kuhakikisha watu wote wanapata mawasiliano.
"Na sehemu yote ambayo watu wanapata mawasiliano maana yake wanaweza kupata masomo ambayo yanatolewa kimtandao na namna nyingine zote katika elimu.
"Ukija katika masuala ya matibabu, ninadhani wote mnafahamu kabisa kwamba TEHAMA inatumika kwa kiasi kikubwa sana kwenye eneo la afya.
"Ili kuhakikisha kwamba watu wanapata huduma za afya au kuweza kufanya shughuli nyingine ikiwemo elimu ya afya.
"Katika masuala ya kibiashara wote tunafahamu kwenye mitandao ya kijamii, mingi sasa hivi inatumika kwenye mambo ya kibiashara.
"Ukija kwenye kutoa huduma mbalimbali ambazo watu wanazipata za Serikali, kwa mfano sasa hivi Serikali ina mifumo zaidi ya 800 inafanya kazi.
"Huduma karibu zote za Serikali sasa hivi zinapatikana kwenye mtandao, kwa hiyo TEHAMA ina faida sana katika sekta mbalimbali.
"Na uchumi wetu unategemea sana TEHAMA, kwa hiyo TEHAMA inagusa sekta zote, utalii TEHAMA ndiyo kila kitu.
"Ukija kwenye usafiri wote tunafahamu kuna huduma mbalimbali zinazotolewa katika TEHAMA, kwa hiyo hii sekta ni ya msingi na sekta ambayo imegusa karibu sekta zote za uchumi za Tanzania," amebainisha Dkt.Mwasaga.
Kuhusu ICTC
Dkt.Mwasaga amesema, Tume ya TEHAMA ilianza kufanya kazi Oktoba, 2015 na ilianzishwa kwa ajili ya majukumu mawili la kwanza ni kuratibu utekelezaji wa Sera ya TEHAMA ya Taifa na la pili ni kukuza TEHAMA.
"Sasa, hivyo vitu viwili ukiviangalia kwa ujumla wake utaona kwamba ni kuhakikisha sekta nzima tunaisimamia.
"Kwa kuhakikisha tuna ratibu utekelezaji wa Sera ya TEHAMA eneo hilo linatufanya tufanye kazi na taasisi zote zilizopo Tanzania.
"Siyo taasisi za umma peke yake, kuna taasisi binafsi na NGOs kwa sababu wote wanaguswa. Tunakuza wataalamu, tunakuza kampuni ndogo ndogo (startups), tunakuza TEHAMA katika mikoa yote ya Tanzania.
"Kwa sasa hivi kuna mikoa ambayo haijaanza kufaidika sana na uchumi wa kidijitali kwa sababu Dar es Salaam ndiyo inapata kwa kiasi kikubwa.
"Lakini, kazi yetu kubwa ni kuhakikisha TEHAMA inaenda mikoa yote na uchumi wa kidijitali unakuwa katika mikoa yote.
"Ikiwezekana katika usawa amabao upo vizuri, lakini cha mwisho ni kuhakikisha kwamba, Tanzania inakuwa shindani kwenye uchumi wa kidijitali ambao ni wa kidunia." Bofya hapa kutazama live mahojiano》》》
Tags
Habari
Kongamano la TEHAMA
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Sekta ya TEHAMA Tanzania
Tume ya TEHAMA