Kortini kwa kughushi cheti cha ndoa ili kupata kadi ya bima NHIF

KILIMANJARO-Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwanyange, Hadija Athumani na Robert Ngowi ambaye ni mfanyabiashara wamefunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Septemba 10,2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Kesi hiyo namba 25889/2024 inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi Mariam Mfanga.

Washtakiwa wanakabiliwa na kosa la kughushi chini ya vifungu 333, 335 na 337 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 Mapitio ya Mwaka 2002 na kuisababisha hasara Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya shilingi milioni 48,364,040.

Ni chini ya Jedwali la 1 aya ya 10 na vifungu 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura 200, Mapitio ya mwaka 2002.

Mshtakiwa namba moja ambaye ni Hadija Athumani anakabiliwa na kosa la tatu ambalo ni kuwasilisha nyaraka yenye maelezo ya uongo kosa chini ya kifungu cha 342 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16 Mapitio ya 2002.

Akisoma hati ya mashtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Eric Kiwia ameieleza Mahakama kuwa mnamo mwaka 2020 washtakiwa walitengeneza cheti cha ndoa cha kughushi ili mshtakiwa wa pili ambaye si mtumishi apate kadi ya bima ya afya kwa ajili ya matibabu yake.

Mshtakiwa namba mbili hakuwepo mahakamani hivyo imechukuliwa hati ya wito ya mshtakiwa chini ya kifungu namba 100 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Masharti ya dhamana ni kuweka nusu ya fedha tajwa ama kuleta hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na fedha tajwa, pamoja na wadhamini wawili wa kuaminika.

Hadi Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU wanatoka mahakamani mshtakiwa wa kwanza alikuwa hajakidhi matakwa ya dhamana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news