Maagizo ya Rais Dkt.Samia yagusa sekta mbalimbali huku akiwashirikisha Watanzania fursa

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikisha wadau mbalimbali na kupendekeza namna bora zaidi ya kushughulikia suala la mmomonyoko wa maadili nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akicheza mchezo wa bao na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati alipotembelea mabanda ya Maonesho katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma tarehe 23 Septemba, 2024.

Ameyabainisha hayo leo Septemba 23,2024 wakati akihutubia katika sherehe za Kilele cha Tamasha la Tatu la Kitaifa la Utamaduni zilizofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.

Pia, Rais Dkt.Samia ametoa wito kwa kila Mtanzania kubeba jukumu la kukagua maadili katika familia yake huku akiwataka viongozi wa kimila na taasisi za kidini kwa pamoja kuungana na Serikali katika kushughulikia mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Jambo hili linaanzia ngazi ya familia, nitoe rai kwa kila Mtanzania kubeba jukumu la kukagua maadili katika boma lake, na ninafurahi kuona viongozi wa kimila mahali hapa.

"Kwa sababu ninaamini kwa kushirikiana na viongozi wa dini tutafanikiwa kushughulikia suala hili la mmomonyoko wa maadili katika jamii."

Mbali na hayo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, Tanzania inatarajia kufungua vituo 100 vya kufundisha lugha ya Kiswahili duniani, hivyo Watanzania wana fursa nyingi za kujipatia ajira na kuimarisha uchumi wao kupitia hatua hiyo.

“Ndugu zangu wana Ruvuma na Watanzania, utamaduni una masuala mengi maana unahusu namna tunavyoishi, kwetu sisi hatuwezi kuongelea utamaduni wetu bila kugusia lugha yetu pendwa ya Kiswahili.

"Ndio lugha inayotuunganisha na kuwa na utamaduni mmoja na lugha hii imefungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania.

"Kwa kuzingatia hili, wizara imenijulisha kwamba mwaka huu wamenijulisha kufungua vituo 100 vya lugha ya Kiswahili kote duniani kwa kushirikiana na Diaspora yetu."

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais Dkt. Samia amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani ambayo imeendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania.

Amesema, mwezi Novemba,mwaka huu tutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Rais Dkt.Samia amesema, kipindi cha uchaguzi ni fursa inayowapa nafasi wananchi kupiga kura ya kupata viongozi watakaowawakilisha katika nafasi mbalimbali za uongozi ili wasaidie kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine amesema, michezo ni sehemu ya utamaduni na jambo la fahari.

Rais Dkt.Samia amewambusha kuwa, Tanzania imepata dhamana kubwa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kuandaa mashindano ya AFCON mwaka 2027.

“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi kuelekea mashindano hayo pamoja na viwanja vingine vilivyopo pia tunafanya ujenzi wa viwanja ambavyo ujenzi unaendelea na ujenzi wa kiwanja kule Arusha unaendelea vizuri.

"Nitoe rai kwa Watanzania kuwa AFCON ni fursa kubwa kwetu kuanzia wajasiriamali wa kazi za ubunifu, utamaduni, sanaa na michezo na Watanzania wote."

Katika hatua nyingine, Rais Dkt.Samia amewataka Watanzania kuwakataa wale wote wanaotaka kuwagawa kwa maslahi yao binafsi, ambapo amesisitiza kutanguliza maslahi mapana ya Tanzania.

“Niwatake Watanzania kutanguliza maslahi ya nchi kabla ya maslahi binafsi, tuwakatae wote wanaotaka kutugawa kwa sababu za kisiasa au tofauti za kiitikadi, Watanzania ni wamoja, Tanzania ni moja, sisi ni mtu mmoja.”

Hata hivyo, katika siku yake ya kwanza ya ziara rasmi mkoani Ruvuma, Rais Dkt. Samia amekagua mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea na kueleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.

“Nimeridhishwa sana na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Songea uliofanyika na kwamba Songea sasa inakwenda kuwa kitovu muhimu cha biashara kwasababu idadi ya wanaokuja Songea imeongezeka sana.”

Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kuchangamkia fursa zinazotokana na uwepo wa Kiwanja hicho cha Ndege cha Songea.

Ameeleza kuwa,tangu mwaka 2021 Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo ya kijamii ikiwemo Shule, Hospitali, Maji pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa itakayokuza uchumi ikiwemo barabara, bandari, Kilimo na Madini.

Mbali na hayo, kwenye ziara hiyo, Rais Dkt. Samia atakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi mkoani Ruvuma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news