DAR-Kufuatia kutofanikiwa kwa maandamano yaliyokuwa yamepangwa na chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wananchi wameendelea kulaani vikali mipango hiyo ambapo wamesema kuwa, suala la maandamano halina tija katika maendeleo ya taifa, hivyo wananchi wajitume ili kukuza uchumi wa nchi
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa, wananchi waache tabia ya kufuata mikumbo kutoka kwa baadhi yao wasio na nia njema, kwani maandamano yamekuwa yakileta hasara kubwa ambapo wametolea mfano maandamano yaliyofanyika nchi jirani ya Kenya.
"Mwananchi usiongozwe na mwenzako, ukafuata akili ya mwenzako kwenda kuandamana sote tumeona nafkiri tumeangalia habari kutoka nchi ya jirani Kenya,wananchi vile wamepoteza maisha na hakuna kitu walichoambulia usifuate ushauri wa mwenzako akakupa ushauri mbaya mkaandamana."
Vilevile wameeleza kuwa, kuna uwezekano mkubwa kuwa CHADEMA hawakufuata sheria katika maandamano hayo na vilevile vijana wamekuwa wakilipwa kwa ajili ya kuandamana kutokana na kukosa kipato, hivyo ni vyema kwa vijana nchini kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka kushawishiwa.
"Inaonekana kabisa CHADEMA hawakufuata sheria mbona mikutano ilikuwa inafanyika enzi na enzi, nchi yetu ni ya amani sasa vichochezi vidogo vidogo visije vikatuweka kwenye sehemu mbaya, vijana wajitume wafanye kazi, ukitaka upate kirahisi ndio mwisho wa siku mnachukuliwa vijana 1,000 mnalipwa kiasi fulani twendeni tukaandameni, mnaanzisha fujo."
Itakumbukwa kuwa, Septemba 11, 2024 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitangaza kufanyika maandamano ya kulaani matukio ya watu kutekwa na mauaji, yakiwemo ya makada wake, lakini Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime lilitangaza kuyapiga marufuku maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika Septemba 23,2024.
Tags
Habari