MUWSA yabisha hodi Marangu Mashariki

 NA GODFREY NNKO

WAJUMBE wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Marangu Mashariki iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wametembelea na kujionea utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa hali ya maji safi unaoendelea ukishirikisha wananchi katika kutunza vyanzo vya maji vya Kerya na Lyasongoro.
Lengo la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Kata ya Marangu Mashariki ambapo eneo hilo linasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).

Mradi huo pia unalenga kuboresha huduma ya maji safi ukiakisi adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Aidha, mradi huo unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 10,574 kutoka vijiji vya Samanga, Rauya na Ashira.

Akitoa taarifa ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Maji wa Maji Safi, Meneja wa Uendelezaji wa Miundombinu, Mhandisi Said Mrindoko amesema kuwa, lengo la kutekeleza mradi huo ni kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama Kata ya Marangu Mashariki.

"Ni katika eneo ambalo linahudumiwa na MUWSA, awamu ya kwanza ya mradi huu utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi milioni 787.2, mradi huu utanufaisha wananchi wa Kata ya Marangu Mashariki katika vijiji vya Samanga, Rauya na Ashira vyenye jumla ya wakazi 10,574."

Aidha, mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili na unatumia fedha za ndani kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).
Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Innocent Lugodisha amesema kuwa, MUWSA imepewa jukumu na Serikali la kuhudumia Kata ya Marangu Mashariki.

"Kwa maana ya kuhakikisha wananchi wa Marangu wanapata huduma ya maji kupitia taasisi hii, ni muda mrefu kidogo ilipewa jukumu hilo na tumekuwa tukifanya kazi mbalimbali kuhakikisha kwamba, wananchi wa Marangu Mashariki wanapata huduma ya maji safi.

"Tunayo mapato ambayo tunayapata kutokana na bili za maji, ambazo zinapatikana kwa wananchi wengine kule mjini, tukasema sasa ni wakati mahususi tutenge mapato ya ndani, twende Marangu Mashariki tukaboreshe huduma ya maji.

"Tumeamua kutenga takribani milioni 780 kwa ajili ya kuviboresha hivi vyanzo na kulaza bomba jipya lenye ukubwa wa nchi nane,hivi vyanzo viwili kimoja litaungwa la nchi sita, lakini yatakutana katikati, itajengwa kituo kikubwa ambacho kitapokea maji kwenye vyanzo viwili."

Mhandisi huyo pia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwatengenezea mazingira mazuri ya wao kufanya kazi zao huku akiwahakiishia wajumbe hao kuwa, fedha hizo zipo.
"Na kwa kweli,hata mwitikio wenu sisi umetutia moyo sana, hasa kwa sisi Kilimanjaro ni Mwenyenzi Mungu mwenyewe aliamua kutubariki akatuweka hapa, akatuwekea mlima huu unatiririsha maji, kwa hiyo watu wa huku watanufaika sana na mradi huu."

Amesema, mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu zaidi ya mahitaji yaliyopo kwa sasa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Marangu Mashariki, Bw.Jonas Mwalla amewashukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kwa kuwashirikisha katika mradi huo.

"Na kutueleza jinsi kazi itakavyofanyika, tulikutana Kamati ya Maendeleo ya Kata, tukiwepo wenyeviti wa vijiji vyote, watendaji wa vijiji vyote, viongozi wa makanisa, mashehe wote waliweza kupata ufahamu kuhusu nini ambacho kinaenda kufanyika katika mrdai huu ambapo MUWSA wameshauanza."

Diwani huyo amesema kuwa, huo ni mradi mkubwa ambao una thamani kubwa ya fedha na wanatarajia unakwenda kumaliza changamoto ya maji iliyopo katika vijiji vya kata hiyo.

Naye, Mchungaji Estomih Urassa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Rauya amesema kuwa, mradi huo ni muhimu kwa wananchi wote.

"Kwa hiyo, hili jambo tulipokee kwa uzito na umuhimu mkubwa sana na wananchi wote wa Marangu waelimishwe vizuri, umuhimu wa jambo hili kwa sababu ni jambo muhimu kwa maisha yao.TAZAMA VIDEO CHINI

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news