ZANZIBNAR-Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mhe.Mama Mariam Mwinyi, Septemba 24, 2024 huko Ford Foundation jijini New York nchini Marekani ameshiriki katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya wake wa Marais wa Afrika (OAFLAD).
Ni kwa ajili ya Kampeni ya #TukoSawa (#WeAreEqual) yenye lengo la kukuza mabadiliko kupitia ushirikiano baina ya wake wa marais barani Afrika.
Mama Mariam alipata nafasi ya kuzungumza na kuonesha yale ambayo taasisi yake ya Zanzibar Maisha Bora Foundation inaunga mkono jitihada za serikali kupitia afua za kimsingi zikiwemo kuwezesha wanawake kiuchumi na kijamii, afya ya msingi pamoja na kupinga udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, hizo pia ndio vipaumbele vya OAFLAD pamoja na elimu ambavyo wake wa marais kutoka nchi 20 wanaungana kuvipambania kwa pamoja.
Aidha, Makamu wa Rais wa OAFLAD Mhe. Denise Nyakéru Tshisekedi, Mke wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alimkaribisha Mhe. Mama Mariam kama mwanachama mpya wa taasisi hiyo na kumuahidi ushirikiano ili kufikia malengo yao ya pamoja.