Mama Mariam Mwinyi atoa uzoefu wa Zanzibar katika elimu Mkutano wa Wake wa Marais Afrika

NEW YORK-Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora, Mama Mariam Mwinyi ameshiriki mkutano wa pamoja na Wake wa Marais wa nchi nyingine za Afrika ambao ni wanachama wa Taasisi ya OAFLAD.
Ni mkutano ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Theirworld umefanyika Septemba 23, 2024 jijini New York nchini Marekani.

Mama Mariam kupitia mkutano huo alipata fursa ya kutoa uzoefu wa Zanzibar kwenye eneo la elimu ya Awali ya Makuzi ya Mtoto (ECD).
Amebainisha kwamba, Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar imefanya juhudi mbalimbali za kutekeleza tamko la kisera iliyobainisha wazi kuwa kila mtoto anayefikia miaka minne ana haki yake ya msingi kupata elimu ya awali.

Pia,Serikali imefanya mapitio ya mtaala kutoka mtaala wa nadharia hadi kuwa mtaala wenye kujenga uwezo wa kiushindani katika elimu na kuanzisha programu ya mlo mmoja kwa skuli za awali za Serikali pamoja na kufanya uchunguzi wa kiafya na kukinga minyoo kwa watoto maskulini kila mwaka.
Vilevile amesema, kwa sasa, Serikali inafanya utafiti wa msingi ili kukuza afua za maendeleo ya mtoto ya awali nchi nzima.
Aidha, kwa upande wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora, katika kuunga mkono juhudi za Serikali, Mama Mariam Mwinyi amesema, imetekeleza Programu ya Lishe kwa kufufua Wiki ya Afya na Lishe inayohamasisha kuzingatia lishe bora pamoja na kuzingatiaj uchunguzi wa kiafya katika hatua za mapema na matibabu kwa watoto zaidi ya 10,000.

Kwa upande mwingine ZMBF inatekeleza Programu ya Tumaini inayozingatia kutoa elimu kwa mtoto wa kike balehe zaidi ya 4,700 ya hedhi salama, lishe na afya ya akili pamoja na taulo za kufua.
Alimalizia kwa kusema kuwa, ili ZMBF iweze kutekeleza programu zake iliyojipangia inahitaji kuungwa mkono na washirika na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news