DAR-Watuhumiwa watano wa usafirishaji wa bangi aina ya skanka kiasi cha tani 1.8, ambao ni Richard Mwanri (47), na mama yake Felista Mwanri (70), pamoja na wengine watatu leo Septemba 10, 2024, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali, Eric Davis amesoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.
Amedai kuwa, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha aina hiyo ya dawa za kulevya kinyume na sheria.
Amesema kuwa, mnamo Agosti 28, 2024, wakiwa eneo la Tairo Luguruni barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo, walikamatwa wakiwa na bangi yenye uzito wa kilogramu 1,815.

Hakimu Mhini amewaeleza washtakiwa kuwa kesi yao ni ya Uhujumu Uchumi, na kwa hivyo hawatapaswa kujibu chochote kwa sasa kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kupokea taarifa kuhusu maendeleo ya upelelezi.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)