Mashindano ya mbio za mbuzi kufanyika Septemba 21,2024 Dar

DAR-Kwa miaka 20, Mbio za Mbuzi zimekuwa zikiwaleta pamoja wadau katika siku iliyojaa furaha kwa lengo la kuchangia miradi ya kijamii, ikiwa ni moja ya matukio ambayo husubiriwa kwa hamu jijini Dar es Salaam.Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay ilichukua hatamu ya kuandaa mbio hizo mnamo mwaka 2018, na mbali na burudani, mbio hizo zina lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya miradi ya elimu nchini Tanzania.

Kupitia mbio hizi, washiriki huungana katika kusaidia wanafunzi wasiojiweza na kuwezesha miradi mbalimbali ya elimu hapa nchini.

Mwaka huu, Mbio za Mbuzi zitafanyika Jumamosi, tarehe 21 Septemba 2024 tofauti na matarajio ya awali ya kufanyika tarehe 7 Septemba.

Mbio hizi zitafanyika kwenye viwanja vya The Green vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 2:00 usiku.

Hii ni mara ya tano kwa Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay kuandaa mbio hizi, ambapo kwa mwaka huu wanalenga kuwa na takribani washiriki 4,000.

Tukio hili ni kielelezo cha moja ya malengo muhimu ya Rotary - kuwaleta wadau pamoja katika kuihudumia jamii.

Mwaka 2023, Mbio za Mbuzi za Rotary zilikusanya zaidi ya TZS milioni 320 kutoka kwa makapuni na watu binafsi walioshiriki katika mbio hizo ambazo huhudhuriwa na watu wa rika zote.

Fedha zinazokusanywa hutumika katika miradi mbalimbali ya elimu, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa masomo kwa vijana wa Kitanzania, kuchangia katika miundombinu ya shule nchini, na miradi mingine ya elimu.
Jitihada hizi ni sehemu ya maeneo muhimu saba yaliyopewa kipaumbele na Rotary International na zinachangia katika miradi inayotekelezwa na Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay, vilabu vingine vya Rotary nchini, pamoja na washirika wa Rotary ndani na nje ya nchi.

Rais wa Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay kwa mwaka2024/25, Himanshu Bhattbhatt, alielezea kuwa mbio za mwaka huu zenye kaulimbiu ya 'Carnival,' zinaendelea kufanya yale ambayo yanaitambulisha zaidi Rotary yaani kukutanisha wadau katika kuihudumia jamii.

“Kaulimbiu ya mwaka huu ni wito kwa wadau wote kukutana na kusherehekea ushirikiano wetu na mafanikio ambayo kwa pamoja tumeyapata katika kusaidia jamii.

"Kwa mara nyingine tena, tumejiandaa kuwa na siku iliyojaa burudani za kutosha kwa lengo la kusaidia jamii na hivyo tunawasihi watu wajitokeze kwa wingi,” alisema Bhattbhatt.

Naye Mratibu wa mbio hizo kwa mwaka huu, Bw. Paul Muhato alisema, “Tuna furaha kuwa na Vodacom Tanzania kama mdhamini mkuu, na tunawashukuru wadhamini wetu ambao wengi wao wanajiunga nasi kwa mara nyingine tena kwa kuendelea kutuamini na kuungana na sisi katika kuandaa mbio hizi.

"Tuna imani kwamba Mbio za Mbuzi za mwaka 2024 zitakuwa zitakuwa kielelezo cha nguvu ya ushirikiano katika kuchangia maendeleo ya elimu Tanzania.

"Washiriki wajiandae kupata kilicho bora kutoka kwa timu yetu, watoa huduma na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.

"Katika maandalizi ya mwaka huu tunashirikiana na wanachama, marafiki na wanafamilia wa Rotary Club of Dar es Salaam Oysterbay, washirika wetu, wauza chakula na vinywaji, serikali ya mtaa na wadau wengineo wengi.​"

Paul aliendelea kwa kueleza kuwa tiketi ya kawaida kwa mtu mzima ni Sh 30,000 na watoto Sh 10,000, huku VIP zikipatikana kwa kati ya Sh 200,000 -250,000 na Sh 30,000 kwa watoto.Mbio za mwaka huu zinaandaliwa kwa udhamini wa mashirika mbalimbali ikiwemo Vodacom Tanzania ambao ni wadhamini wakuu, EATV, Tanzanite Dream, YARA, Toyota, Pepsi, GardaWorld, Abstrat PR & Marketing, RedNWhite, TBL, Trellidor,

JC Decaux, Slipway, Bowmans Law, Oryx. Energies, Pesapal, Le Grande Casino, Bobo, Premier Care, Jibu, na Minet.

Kampuni hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha mbio za mwaka huu zinafana kupitia mchango wa fedha taslimu na huduma/bidhaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news