DAR-Matumizi ya Teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya asilimia 70.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila alipotembelea banda la TARURA kwenye Maadhimisho ya 21 ya Siku ya Wahandisi katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

"Ujenzi wa madaraja na barabara kwa kutumia teknolojia ya mawe unapunguza gharama kwa asilimia 70 ukilinganisha na zege lakini pia tuna teknolojia ya kutumia kemikali kuboresha udongo unaopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi,"amesema.
Ameongeza kwamba,TARURA imeweza kuondoa vikwazo sehemu zisizopitika kwa kujenga madaraja ya gharama nafuu kwa kutumia teknolojia mbadala hasa maeneo ya vijijini na kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi zaidi.
