Mawakili waja na mwelekeo chanya kwa ustawi bora wa Taifa

NA GODFREY NNKO

UJUMBE kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Chama Cha Mawakili wa Serikali (PBA) umefanya ziara katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha na kuweka mikakati ya kufanya kazi kwa ustawi bora wa Taifa.
Ziara hiyo imefanyika leo Septemba 25,2024 katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam ambapo vyama hivyo kwa upande wa TLS umeongozwa na Rais Boniface Mwabukusi na upande wa PBA umeongozwa na Rais Amedeus Shayo. Aidha, ujumbe huo umepokelewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.Ally Possi.

Wakili Mkuu wa Serikali

Wakili Mkuu wa Serikali,Dkt. Ally Possi amesema, ugeni huo ni muhimu si tu kwa ofisi yake bali kwa ustawi wa Taifa na jamii kwa ujumla.
"Leo ofisi yetu tumepata ugeni wa vyama hivi viwili muhimu ambavyo sisi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tunatambua kazi kubwa vinavyofanya kwa njia moja ama nyingine na kutokana na shughuli ambazo tunazifanya nyingi zikiwa ni za kimahakama.

"Nyingi ni za kuwasaidia wananchi ambao ni wateja wetu, zote zikiwa ni za kisheria ambazo wote tunafanya tumeona kuna haja ya kushirikiana na kuangalia mawanda ambayo sisi kama wanasheria wa Tanzania tunaweza tukashirikiana

"Kwa hiyo, Public Bar na TLS tayari wameshaandaa Memorandum of Understanding ambayo itapitia taratibu za Serikali na utakapokamilika basi tutasainishana."

Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi amesema, kilichopo katika MoU hiyo ni kuhusu suala la taaluma na mambo mbalimbali.

"Dunia imebadilika, tuna uwekezaji wa Kimataifa si tu kwa mwekezaji kuja Tanzania, lakini wawekezaji wetu kwenda nje ya Tanzania.

"Sasa hatutaki, mwekezaji anatoka nje ya Tanzania anatumia mwanasheria wa kigeni, wanasheria wa Tanzania wapo.Law Schools zipo na zinatoa wahitimu wanasheria ambao ni Watanzania.

"Kwa hiyo, moja ya mambo ambayo tunataka kushirikiana ni kukuza taaluma kwa wanasheria ambao wamehitimu ambao wamesoma, wote ambao wapo katika sekta ya Sheria.Kwa hiyo, ni jambo ambalo tutalifanyia kazi.

Dkt. Ally Possi amesema, jambo la pili ni kuendeleza maadili ya wanasheria kwa ujumla wake nchini.
"Kwa sababu, maadili ni jambo mtambuka na ni endelevu. Dunia inabadilika, utandawazi unakuwa, lakini pia kama tunavyofahamu Duniani tuna-deal na utakatishaji wa fedha.

"Na sisi wanasheria tuna jukumu hilo la kuhakikisha kuwa, yale mambo ambayo yatahujumu uchumi wa nchi na mambo ambayo yanahusishwa na Sheria kwa namna moja ama nyingine aidha kwa kuingia mikataba.

"Aidha, kwa kusaidia kufanga miamala ambayo itahujumu uchumi wa nchi yetu basi ni jambo ambalo tutahakikisha TLS, Public Bar na wanasheria kwa ujumla wa nchini kwetu tunaepuka na tutahakikisha kuwa, tunasimamia maadili ya mawakili."

Jambo la tatu, Wakili Mkuu wa Serikali ameeleza ni kufanya kazi kwa karibu na Mahakama.

"Utatuzi wa migogoro nje ya mahakama ni mambo ambayo yatasaidia kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

"Lakini, itasaidia pia kutatua matatizo ya wananchi kwa haraka kwa sababu unapokuwa na kesi nyingi mahakamani mathalani, kesi inachukua mwaka mmoja, miaka miwili jambo ambalo kumbe tungeweza kukaa mezani takribani wiki mbili, wiki moja, siku tatu zile changamoto ambazo wananchi au mwananchi anapambana nazo tungeweza kuzitatua.

"Kwa hiyo ni mambo ambayo tumeyajadili, na tutayaweka katika huo ushirikiano na tutafanya kazi kwa pamoja."

Aidha, Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa, wameangazia namna ya kuangalia fursa zilizopo katika nchi jirani, kanda na Kimataifa.

"La mwisho ambalo tumejadiliana ni namna bora ya kusaidia Serikali katika kutoa ushauri ambao utaisaidia nchi yetu na kuisaidia Serikali kwa ujumla.

"Kwa hiyo, tutaweka namna bora za kuwatambua wenzetu mawakili binafsi ambao wana mchango mkubwa.

"Lakini, pia namna bora ya kuwashirikisha katika shughuli za kiserikali, lakini pia namna bora mawakili ambao wanafanya kazi Serikalini pia ya kuisaidia sekta binafsi.

"Sisi ni wabobezi wa sekta zote ambazo zipo zinaendelea, mafuta na gesi, mambo ya kodi, madini lakini pia mikataba hata uandishi wa Sheria,"amesisitiza Wakili Mkuu wa Serikali,Dkt. Ally Possi.

Rais wa PBA

Kwa upande wake Rais wa PBA,Amedeus Shayo amesema kuwa, "Nishukuru kwa kupata fursa ya kukutana na Wakili Mkuu wa Serikali kama alivyoeleza lengo letu lilikuwa kwanza kama mtakumbuka Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati akizindua chama chetu tarehe 22 mwezi wa 9, 2022 alitoa agizo.
"Aliagiza na akasema kwamba ninyi mawakili ni jeshi, nyie ni jeshi la kalamu na karatasi tumieni hizo nyenzo kulinda uchumi wetu, kulinda biashara na uwekezaji.

"Kwa hiyo, lengo letu kukutana hapa leo lilikuwa ni pamoja na mambo mengine kuangalia ni jinsi gani tunaweza kutekeleza agizo hilo,"amebainisha Rais wa PBA,Amedeus Shayo.

TLS

Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi akizungumzia kuhusu ziara hiyo amesema kuwa,"Sisi Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) tukiongozwa na Baraza la Uongozi tumefika katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa nia kubwa,kwanza ya kujitambulisha na kusalimia ili kufahamiana.

"Lakini, vile vile kukutana na wenzetu ambao vile vile tuna kiongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali, wote tumekutana nao hapa na lengo letu kubwa kwa siku ya leo ilikuwa kufahamiana na tumezungumza masuala kadhaa.

"Kwa sababu kama mnavyoelewa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ndiyo washauri na watendaji kwenye masuala ya kisheria kumsaidia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na katika kuendesha mashauri mbalimbali.

"Na sisi kama mnavyofahamu kama nawakili vile vile kazi yetu kubwa ni mahakamani ndiko tunakoendesha mashauri.

"Tumezungumzia mambo mengi ya msingi na ni namna gani tutaitumia taaluma yetu kwa maslahi ya Taifa, maslahi kwa uwekezaji.

"Lakini kuhakikisha kwamba uwepo wa TLS na uwepo wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali unakuwa na tija na faida zaidi kwa Serikali."
Rais Boniface Mwabukusi amesema, pia wamekubaliana maeneo ya kushirikiana na moja ya maeneo ni namna ya kushirikiana kati ya wao TLS na wenzao wa PBA.

"Ni katika kushirikishana uzoefu, kujengeana uzoefu na katika kutekeleza majukumu yetu kwa namna ambayo itakuwa na tija kwa Taifa na itakuwa na tija kwa shughuli zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazoendelea katika taifa letu.

"Kwa hiyo moja ya mambo tuliyozungumzia ni kuhusu kusaini makubaliano kwa maana ya Memorandum of Understanding (MoU) kati ya TLS na wenzetu wa Public Bar.

"Na kwa namna ya kuhusiana namna ya kufanya shughuli zetu, namna ya kujengeana uwezo na namna ya kushirikishana uzoefu katika masuala mbalimbali.

"Vile vile tumeweza kuzungumza kuweza kuona namna bora ambavyo tutaweza kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Proactive ninaposema Proactive ni kushirikiana kwa namna ya kujenga.

"Kwa sababu kuna kushirikiana kwa namna ya kukosoa ninaweza kukusubiri ufanye ukosee nikushambulie, lakini kwa namna bora ya kujenga kwa namna ya usimamizi wa sheria zetu za ulinzi wa rasilimali na uendeshaji wa rasilimali zetu.
"Hapa tunazungumzia Sheria Na.5 na Na.6 kuona ni namna gani tutashirikiana kwa ubora, kuona kwamba maudhui au dhima iliyowekwa katika uandikaji au kusudio la uwepo wa sheria zile nzuri unakuwa na tija kwa Taifa katika masuala ya uwekezaji, katika masuala ya utatuzi wa migogoro na usimamizi wa rasilimali za Taifa.

"Kwa hiyo ni maeneo ambayo tulifikiri tutashirikiana na kuona namna bora ambavyo tutakuwa tuna uwezo wa ku-engage na kuishauri Serikali yetu katika hatua zote za kimichakato, za mikataba.

"Lakini vilevile tumeweza kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu namna ya kuzipa nguvu sheria hizi ikiwemo utatuzi wa migogoro ya uwekezaji kuifanyia ndani ya nchi.

"Yaani badala ya kwenda kutatua matatizo nje ya nchi, ni kwamba tuwe na mfumo wetu tuweke mechanism yetu tuone namna tutakavyoweza ku-harmonize kuona namna bora ya kusuluhisha migogoro inayotokana na uwekezaji katika rasilimali zetu na wawekezaji.

"Nia yetu ni kwamba, uwepo wa TLS na uwepo wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na wenzetu wa Public Bar iwe sasa ni daraja la kuhakikisha tunapofanya shughuli za uwekezaji Taifa linafaidi,mwekezaji anafaidi, lakini maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho cha Taifa hili yanalindwa na katika uwepo wa rasilimali hizo,"amefafanua kwa kina Rais wa TLS,Boniface Mwabukusi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news