MANYARA-Mbunge wa Jimbo la Kiteto mkoani Manyara, Mheshimiwa Edward Ole Lekaita amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kuwa, Rais Dkt.Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ambapo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika Jimbo la Kiteto umeongezeka.
Mbunge Ole Lekaita ametoa pongezi hizo Septemba 7,2024 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndirigishi mara baada ya kuzindua shule mpya ya Sekondari ya Ndirigishi.
Amesema kuwa, kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Dkt.Samia anaenda kuandika historia kubwa katika Jimbo la Kiteto na nchi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa, katika uongozi wa Rais Dkt.Samia shilingi bilioni 1 imetolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule na mabweni katika shule hiyo ya Sekondari ya Ndirigishi.
Shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo vya Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kiteto, shilingi bilioni 1 kwa ajili wa ujenzi wa soko la mazao Engusero na shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Hali kadhalika, Mbunge Ole Lekaita amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha upatikanaji wa umeme katika vijiji vyote katika Wilaya ya Kiteto.
Pia amesema kuwa, zaidi ya madarasa 200 yamejengwa katika kipindi cha uongozi wake huku shule shikizi 18 zikiwa zimejengwa na kusajiliwa huku shule mpya mbili za msingi zikiwa zimejengwa katika Kata ya Matui na Dongo.