DAR-Wajasiriamali wadogo wapatao 500 wanaojihusisha na uchimbaji na uchakataji kokoto jijini Dar es Salaam wamewezeshwa vifaa kinga na kupatiwa mafunzo ya usalama na afya ili kujiepusha na ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vilivyopo katika mazingira ya kazi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mary Maganga amesema kwa kuzingatia mchango wa wajasiriamali wadogo katika maendeleo ya nchi, OSHA imeona ni muhimu kuwapa elimu ya usalama na afya wachimbaji hao ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo yanayotolewa na wataalam wake kwa wachimbaji wadogo yamejikita katika kuwawezesha kutambua vihatarishi vinavyoambatana na shughuli zao ikiwemo vumbi, joto kali na mtindo wa ufanyaji kazi usiozingatia taratibu za igonomia.
Vifaa kinga vilivyotolewa kwa wajasiriamali hao ni pamoja na barakoa, vikinga mikono (gloves), vizibao vinavyoakisi mwanga (reflective vests) kutambulisha uwepo wa mfanyakazi mahali pa kazi pamoja na masanduku ya huduma ya kwanza.

Wajasiriamali walionufaika na uwezeshaji huo wameishukuru serikali kupitia OSHA kwa mafunzo ya usalama katika maeneo ya kazi na uwezeshaji wa vifaa kinga walivyopata.