Mhasibu wilayani Mtama hatiani kwa rushwa

LINDI-Mhasibu Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama,Bakari Issa Ngumba leo Septemba 3,2024 amefunguliwa kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.
Mshitakiwa anakabiliwa na makosa mawili ambayo ni kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri Kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 32 Marejeo ya Mwaka 2022.

Ni kifungu ambacho kinasomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la kwanza pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 Marejeo ya mwaka 2022.

Kosa lingine ni kughushi kinyume na kifungu cha 333,335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya Mwaka 2022.

Imedaiwa,mshitakiwa akiwa Mhasibu Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, kati ya tarehe 31 Desemba 2021 na 31 Januari 2022, alighushi orodha ya malipo pamoja na hati ya malipo.

Ni hati inayoonesha kuwa, alimlipa dereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kiasi cha shilingi 650,000 kama malipo kwa ajili ya kazi ya usimamizi wa miradi ya maendeleo vijijini jambo ambalo halikuwa kweli.

Aidha,mshtakiwa aliwasilisha nyaraka hizo zilizoghushiwa kwa mwajiri wake ili aidhinishe malipo hayo.

Baada ya kusomewa hati ya mashtaka mshtakiwa alikana makosa yote mawili na akakamilisha masharti ya dhamana.

Hata hivyo,kesi imepangwa kuja kwa kusomwa hoja za awali Oktoba 2,2024.

Kesi hii inaendeshwa na Wakili wa Serikali Salum Bhoki kutoka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news