DODOMA-“Nimekuja kujifunza na kuhimiza masuala ya uadilifu, uzalendo na namna bora ya kutoa huduma kwa umma, kwa kuwa watumishi wa mamlaka hii wanawajibu wa kusanifu, kujenga na kusimamia mifumo ya TEHAMA Serikalini ili Serikali iweze kutoa huduma kwa umma kwa urahisi, haraka na gharama nafuu”.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akisalimiana na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati alipowasili katika ofisi hiyo kwa ziara ya kikazi jijini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu Septemba 5, 2024 jijini Dodoma wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) lengo la kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanya kazi na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyofanyika jijini Dodoma.
Mhe. Sangu alieleza kuwa Mamlaka ya Serikali ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa, hivyo watumishi wake hawanabudi kuzingatia misingi ya uadilifu na uzalendo kwa kuwa taarifa nyingi za Serikali zinapita katika mifumo waliyoijenga na wanayoisimamia.
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Dodoma.
Aidha, aliongeza kwa kutoa pongezi kwa watumishi wa eGA kwa kuifanya Serikali kuwa ya kidijitali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma, mathalani mifumo iliyosanifiwa na kujengwa na eGA imeondoa upendeleo katika ajira za Serikali, wananchi wanaweza kulipia na kupata huduma mbalimbali wakiwa mahali popote na kwa wakati wowote.
Baadhi ya Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi.
Pia, alisisitiza watumishi wa Mamlaka hiyo kuendelea kuhimiza taasisi za umma kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa lengo la kuimarisha usalama wa mifumo ya Serikali na ya sekta binafsi iliyounganishwa na Serikali.
Katibu Mkuu-IKULU, Bw. Mululi Majula Mahendeka akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu kuzungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyofanyika jijini Dodoma.
Awali, Katibu Mkuu-IKULU Bw. Mululi Majula Mahendeka alisema kuwa watumishi wa eGA wanatakiwa kufanyakazi kwa weledi na uadilifu ili kuifanya mifumo ya Serikali kuwa imara na inayoaminika kwa wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba akielezea mafanikio na utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyofanyika jijini Dodoma.
Vilevile, Mkurugenzi Mkuu wa eGA,Mhandisi Benedict Ndomba alisema kuwa pamoja na mambo mengine mamlaka imeshirikiana na taasisi husika kujenga Mfumo wa kielektroni wa Usimamizi wa Vyama vya Ushiriki (MUVU) ambao unarahisisha ukaguzi, usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika ili kuboresha utendajikazi, kuchochea mabadiliko ya kiuchumi na kuongeza uwazi.