Mkutano wa Kimataifa kuhusu haki na mazingira wahitimishwa Rwanda

Na FAUSTINE KAPAMA
Mahakama ya Tanzania

MKUTANO wa Kimataifa uliokuwa unafanyika jijini hapa kuzungumzia haki mazingira uliowaleta pamoja Majaji na Mahakimu kutoka Jumuiya ya Madola umehitimishwa leo tarehe 11 Septemba, 2024.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akijadiliana jambo na Jaji Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Faustin Ntizilyayo kwenye Mkutano huo leo tarehe 11 Septemba, 2024.

Akizungumza katika hafla fupi, Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Lynne Leitch amesema Mkutano huo umekuwa wenye mafanikio makubwa na amepokea taarifa nyingi kutoka kwa washiriki kuwa elimu waliyoipata imevuka matarajio waliyokuwa wanategemea.

Ameipongeza Serikali na Wananchi wa Rwanda kwa kuonesha ukarimu wa hali ya juu kwa kipindi chote cha Mkutano tangu ulipofunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame tarehe 9 Septemba, 2024.

Mhe. Leitch ameishukuru pia Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo kwa kazi nzuri iliyofanya iliyowezesha shughuli zote kufanyika kama ilivyopangwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akijadiliana jambo na Jaji Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Faustin Ntizilyayo kwenye Mkutano huo leo tarehe 11 Septemba, 2024.

Kabla ya kuhitimishwa mkutano huo, washiriki kutoka Mataifa mbalimbali walijadili mada kadhaa, ikiwemo iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi atawasilisha mada kuhusu “upokeaji wa ushahidi unaotokana na kompyuta.”

Mada zingine zilikuwa ni mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mahakama iliyowasilishwa na kujadiliwa na Jaji Mariama Owusu kutoka Gambia, Jaji Dyakatonda John kutoka Rwanda, Bw. Neil McCallum kutoka Uingereza na Wales na Bi. Nyambura Mbatia kutoka Mahakama ya Comesa.

Baada ya hapo, wajumbe waligawanyika kwenye makundi na kujadili mada mbalimbali, ikiwemo kwamba kama Mahakama inaweza kusema au kutenda jambo lolote mbele ya umma.

Baadaye washiriki walijumuika tena pamoja kupokea mada iliyowasilishwa na Jaji kutoka Tanzania na kujadiliwa na Bw. Thomas Brewer kutoka Uingereza na Wales, chini ya uenyekiti wa Jaji Rangajeeva Wimalasena kutoka Nauru.
Majaji kutoka Tanzania (juu na picha mbili chini) wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa kwenye Mkutano huo. Picha ya chini wa kwanza kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, akiwa na Viongozi Waandamizi wa Mahakama (waliopo nyuma yake).
Hapakuwepo na maswali menage yaliyoulizwa na washiriki katakana na umahiri na uelewa wa kutosha uliooneshwa na Jaji kutoka Tanzania wakati wa uwasilishaji wa mada hiyo.

Wakati wote wa Mkutano, jumla ya mada 18 ziliwasilishwa, ikiwemo iliyowaslishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Ilvin Mugeta kuhusu utoaji wa adhabu kwenye kesi za utoroshaji wa wanyamapori.

Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliongozana na Majaji wawili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na Majaji wengine wa Mahakama Kuu, Mhe. John Kahyoza, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), Mhe. Ilvin Mugeta, Mhe. Butamo Philip, Mhe. Yohana Massara na Mhe. Dkt. Adam Mambi.

Viongozi wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi, Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Aidan Mwilapwa na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Dkt. Jovin Bishanga.
Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar (wa kwanza kulia) akifuatilia matukio mbalimbali. Picha ya chini wa pili kutoka kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara na Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. John Kahyoza.
Sehemu ya Viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa wakati wa Mkutano huo.

Walikuwepo pia Viongozi wa JMAT, Mhe. Shaibu Mzandah, ambaye ni Makamu wa Rais, Mhe. Lazaro Magai, ambaye ni Katibu Mkuu, Mhe. Mary Kallomo, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu na Mkuu wa Secretariat, Mhe. Nemes Mombury, ambaye ni Katibu Mwenezi na Mhe. Devota Ksebele, ambaye ni Mweka Hazina na Mahakimu wengine, Mhe. Adeline Kashura na Mhe. Hassan Chuka, ambaye pia ni Katibu wa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Haki Mazingira” uliandaliwa na Jumuiya ya Madola kwa kushirikiana na Mahakama ya Rwanda.

Wakati wa Mkutano, Majaji na Mahakimu walijadili vipengele mbalimbali vya kisheria na kitaasisi ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa haki kuhusiana na mazingira na jukumu kuu la Mahakama katika kudumisha haki mazingira.

Kupitia mada na mijadala mbalimbali, wajumbe wa Mkutano huo walipata fursa za kubadilishana uzoefu kati yao na kuunda uhusiano wa kudumu miongoni mwao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news