IRINGA-Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amewataka wakandarasi wanaojenga mradi wa Umwagiliaji Skimu ya Mkombozi mkoani Iringa kuongeza kasi.
Ni katika ujenzi wa miradi hiyo ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali unanufaisha wakulima katika msimu ujao.Amewataka wakandarasi hao kuwa na mkakati wa kumaliza ujenzi wa miradi hiyo hadi kufikia mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza katika vikao kazi baina ya uongozi wa Tume na wakandarasi hao mkoani humo, Mndolwa amesisitiza wakandarasi hao wafanye kazi usiku na mchana kumaliza mradi kwa wakati.
Wakandarasi wanaojenga mradi wa Mkombozi lot I na lot II unaofanywa na kampuni ya ndani ya Cimfix & Engineering, sambamba na ujenzi wa mradi Mkombozi lot III na lot IV unajengwa na kampuni ya CRJE Engineering kutoka China
Mndolwa pia ameongoza kikao kazi baina ya Tume na Mkandarasi ujenzi wa Mkombozi M/S Cimfix& Engineering Co Ltd kilichofanyika katika kambi ya Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Mkombozi lot I na II mkoani Iringa.
Katika kikao kazi hicho kilichoambatana na ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na NIRC, Mndolwa ametoa maelekezo mbalimbali yaliyolenga kutaka matokeo yenye tija na mradi kukamilika kwa wakati.
Mkandarasi aliwasilisha mkakati wa kumaliza mradi kwa wakati, ambapo kazi kubwa zilizobaki zitaanza tarehe 6 Septemba na kukamilika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Wajumbe walipitia mkakati huo na kutoa maoni na maazimio, huku mkandarasi akikubali kufanya marekebisho ya mpango kazi ili kuendana na mabadiliko yaliyojadiliwa.
Katika ukaguzi wa miradi ya Lot I & II, maagizo mbalimbali yalitolewa, ikiwemo kufanya utafiti wa kurudisha mto katika mkondo wake wa asili na kujenga bwawa ili kulinda miundombinu.
Sanjari na hayo, usanifu wa mfereji utabadilishwa kutoka mfereji wa wazi kuwa uliofunikwa, na tuta la barabara litapandishwa ili kuzuia uharibifu wa miundombinu kutokana na mafuriko.
Timu ya wataalam wa Tume imeundwa na itaanza kazi tarehe 09/09/2024.
Pamoja na hayo,Maboresho katika eneo la banio ni pamoja na kuongeza urefu wa gabions, kuweka guardrails, na kujenga kibanda kwenye jiwe la msingi.
Pia, eneo la banio litafanyiwa usawazishaji, kuwekwa paving, fensi, na alama za barabarani, huku miti ikipandwa kwenye barabara zote zilizolengwa
Mradi wa Mkombozi unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kupitia Mkandarasi M/S Cimfix&Engineering Co Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 56, ambapo eneo la hekari 15,000 litawekewa Miundo mbinu ya umwagiliaji na utanufaisha jumla ya watu 21206.
Katika hatua nyingine Mndolwa akizungumza na viongozi wa Kampuni ya CRJE kuhakikisha kasi ya ujenzi wa mradi inaongezeka na uweze kukamilika.
Pia ainishe mahitaji ya utekelezaji wa mradi ili kujua thamani ya fedha zinazohitajika ili kusiwe na vikwazo vya kikamilisha miradi hiyo.
Pia, alihimiza haja ya utambuzi na upimaji shamba la Mkombozi na kulipatia hati miliki shamba.Kufanya maandalizi ya kusafisha shamba Shamba la Mkombozi.
Meneja wa mradi alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi ya LOT III na LOT IV ambapo mpaka sasa, LOT III imekamilika kwa 33.6%, wakati LOT IV imefikia 82.2% ya ukamilishaji.
Kikao hicho kilimuagiza mkandarasi kulenga angalau 95% ya ukamilishaji kwa LOT zote mbili ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2024.
Kwa upande wa Mkandarasi wa CRJE, Zhang Lin Jie amesema wamepokea maagizo hayo na lengo hili mbele ya Meneja wa mradi pamoja na uongozi wa Tume ,ambapo wote kwa pamoja walipanga rasilimali na vifaa vinavyohitajika kufikia lengo hili.
Naye Meneja wa Mradi, Peter Akonaay alisisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya kiufundi yaliyojadiliwa na kumuhimiza mkandarasi kuyachukulia kwa uzito.
Tags
Habari
Kilimo cha Umwagiliaji
Skimu ya Mkombozi mkoani Iringa
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC)