Naibu Waziri Sangu atoa maelekezo TAKUKURU, asisitiza haki na uadilifu

NA LUSUNGU HELELA
Tabora

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa mfano kwa kujipambanua kutenda haki na kuonesha uadilifu katika jamii huku akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa Mtumishi yeyote wa TAKUKURU atakayebainika kuwa sio muadilifu.Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo mara baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa ofisi za TAKUKURU Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora uliogharimu kiasi cha Sh. Milioni 314.2 hadi kukamilika kwake.

Amesema, TAKUKURU ni chombo kinachohitaji watumishi wenye uadilifu wa hali ya juu hivyo kwa Mtumishi yeyote ambaye sio muadilifu TAKUKURU si mahali sahihi kwa yeye kufanya kazi.

Amesema, ni jambo lisilokubalika kwa chombo hicho cha kuzuia rushwa halafu kukawa na Watumishi mabingwa wa kupokea rushwa.
Akizungumzia ujenzi wa ofisi hiyo, Mhe. Sangu ameipongeza TAKUKURU kwa kuonesha mfano namna fedha za Watanzania zinavyotakiwa kutumika kwani thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa ofisi hiyo inaonekana.

"TAKUKURU ni chombo kinachosimamia uadilifu na kinatakiwa kiwe cha kwanza kuonesha uadilifu kwa matendo yake, kwa namna nilivyokagua jengo hili nimeridhishwa mno naamini wateja wetu watakaokuja hapa kwa ajili ya kuchunguzwa hili jengo litumike kama mfano kwa kuonesha thamani ya fedha iliyotumika,"amesisitiza Mhe. Sangu.
Hata hivyo, Mhe. Sangu ameiagiza TAKUKURU kuhakikisha inahamia katika ofisi hiyo ya kisasa ndani ya mwezi huu ikizingatiwa kuwa ofisi wanazozitumia kwa sasa katika Wilaya hiyo kodi yake ya pango itafikia ukomo mwezi huu.

Amesema, kukamilika kwa Ofisi hiyo kunaonesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha TAKUKURU inawajibika ipasavyo kwa wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kukubali kutoa fedha hizo ili kuhakikisha Watumishi wa Takukuru katika Wilaya ya Nzega wanatimiza wajibu wao kwa kufanya kazi katika Ofisi nzuri na za kisasa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Sangu ameitaka TAKUKURU kuzifanyia kazi kwa wakati nyaraka za mikataba ya miradi ya maendeleo ambazo huwasilishwa kwao kutoka kwa Wateja wao.
Amesema kama jambo limekamilika au halina uchunguzi wowote ni muhimu nyaraka hizo zikarudishwa haraka kwa wahusika badala ya kukaa nazo kwa kipindi cha muda mrefu kwani lengo la TAKUKURU kupewa nyaraka hizo ni kuzuia rushwa ili kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inapoanza kutekelezwa isiharibike.

Amesisitiza kuwa, ni muhimu kwa nyaraka hizo za mikataba kufanyiwa kazi ipasanyo ili kuhakikisha miradi hiyo ya maendeleo inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuonesha thamani ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news