Namna ambavyo kuwa mwema sana kwa kila mtu kunaweza kuyaweka maisha yako hatarini

NA SAID KASEGE

KAMA utafuatilia mafundisho mbalimbali huwa kuna msisitizo mkubwa sana kwa jamii kuhusu kutenda wema, kusaidia sana watu,kuwa mstaarabu,kuepuka migogoro,kuepuka kukasirika, kusamehe makosa ya watu wengine,kuwa mvumilivu juu ya mapungufu ya watu wengine n.k.
Picha na ingrid.

Pamoja na hivyo umewahi kujiuliza madhara ya kujihesabu kama mtu mwema sana katika jamii?, umewahi kujiuliza madhara ya kutaka kuonekana mtu mwema sana kuliko watu wote katika jamii.

Kisaikolojia binadamu huwa anaishi kwa mazoea kwa mfano endapo wapendwa wako wamezoea kuona unawapa zawadi kila siku wataamini zawadi ni haki yao na endapo utashindwa kuwapa zawadi watakuchukia hata kama upo na dharura au upo na matatizo ambayo yapo nje ya uwezo wako.

Vilevile kama Watu wamezoea kuona unatanguliza maslahi yao kabla ya kujali mahitaji yako siku ambayo utabadilisha utaratibu watakuchukia sana japokuwa siyo kosa.

Kama Watu wamezoea kuona hauna hasira,unasamehe kila kosa, unavumilia tabia zenye maudhi,upo tayari kukopa ili kujali mahitaji ya watu wengine siku ambayo utabadilisha utaratibu watakuchukia sana japokuwa mtu mwengine ambaye hana utaratibu wa kujali mtu yeyote akifanya hivyo Watu wanakaa kimya.

Watu wakizoea kwamba chochote ambacho watakwambia utakubaliana nao bila kuhoji chochote watazoea kukupangia namna ya kuendesha maisha yako lakini siku ambayo utahoji utapigwa vita na watakuchukia sana japokuwa kwa mtu ambaye amekuwa na tabia ya kuhoji watakaa kimya.

Ugomvi baina yako na wapendwa wako utaibuka kwa sababu ya mazoea ambayo wamejenga juu yako.

Ukiwa mgomvi mgomvi siku ukiwa mpole kupitiliza, mkarimu sana,unasaidia sana watu wengine ghafla wapendwa wako watakuwa na taharuki siyo kwa sababu ya wema wako bali kwa sababu siyo tabia yako.

Soma ujumbe mpaka mwisho.

Leo tuangalie madhara ya tabia ya kutaka kuonekana mwema kwa kila mtu namna tabia hiyo inaweza kuyafanya maisha yako kuwa magumu sana.

Kwa kawaida mtu ambaye huwa anasifika kuwa ni mwema sana katika jamii huonyesha tabia zifuatazo anakuwa mpole, mcheshi,anasamehe makosa , mvumilivu,anajitoa mhanga kusaidia sana watu katika jamii,mnyenyekevu,anakuwa na huruma, haonyeshi hasira,hapendi migogoro wala ugomvi.

Sifa hizo hapo juu ni nzuri sana kuwa nazo lakini kuna madhara ndani yake endapo utakuwa unataka sifa hizo ziwe utambulisho wako kila sehemu- mbele ya kila mtu.

Kwa maana hautaki kusikia unatajwa kwa sifa tofauti na hizo.Sifa hizo nzuri kwako zinageuka gereza kwako mwenyewe katika vipengele vifuatavyo.

MADHARA YA TABIA YA UNYENYEKEVU, UVUMILIVU, HURUMA NA KUSAIDIA SANA WATU KATIKA JAMII BILA KUJIWEKEA MIPAKA

Sifa za huruma, kujali, kunyenyekea, kusamehe makosa, kujitoa mhanga, kusaidia sana watu, uvumilivu zinaweza kuyaweka maisha yako hatarini kama utaonekana na sifa hizo mbele ya kila mtu kwa njia zifuatazo.

1.MATARAJIO AMBAYO SIYO HALISI

Kwa sababu utakuwa na sifa za upole, huruma, kujali, kunyenyekea, kusamehe makosa, uvumilivu, kujitoa mhanga, kusaidia sana watu wengine katika jamii utaamini kwamba watu wote katika jamii ni wema sana,wenye huruma, wastaarabu, wavumilivu sana kama ilivyo wewe na utakuwa na matarajio ya kutendewa kama vile ambavyo wewe unatenda kwa watu wengine lakini inakuwa kinyume chake.

Ukiamua kuwa mwema sana katika jamii haina maana kwamba wahalifu wataacha uhalifu,wezi wataacha kuiba, Watu wengine wataacha kusaliti wenza wao,haina maana kila mtu atakuwa mvumilivu,haina maana kila mtu atakuwa muelewa Lah.

Kila mtu atabaki na tabia zake bila kujali tabia yako ikoje.

Ukiwa mwema unakuwa mwema kwa ajili ya nafsi yako na ukiwa mbaya unakuwa mbaya kwa ajili ya nafsi yako sio vinginevyo.

2.WATU WATAKUONA DHAIFU SANA IKIWA UTAOGOPA MIGOGORO

Kwa sababu utakuwa hautaki kuonekana mbabe, mgomvi,mchoyo, mbinafsi n.k utalazimika kusamehe makosa ya kila mtu, utalazimika kujitoa mhanga kwa kila mtu, utalazimika kuacha kazi zako ili kuwafurahisha Watu wengine,utaacha ratiba zako kwa ajili ya kujali ratiba za Watu wengine lakini wao hawawezi kuacha kazi zao kwa ajili ya kazi zako hata ikitokea dharura.

Kwa sababu watafanya hivyo ? Ni kwa sababu wanajua utasamehe tu haijalishi watafanya makosa mara ngapi,utavunjiwa heshima mara kwa mara kwa sababu wengine watakuwa wanakupima msimamo wako.

Mara kwa mara utaona mwenza wako na watoto wako wanakugombeza,wanakufokea,wanakutoa dosari za muonekano mara kwa mara,wanakujibu vibaya lakini utakuwa unapuuza.

Kwa sababu unajitoa mhanga kila wakati utajikuta umezungukwa na watu ambao wanataka msaada wako lakini hawana uwezo wa kukusaidia kwa jambo lolote hata ukiwa na dharura.

Kwanini itakuwa hivyo? Ni kwa sababu uliamini ukiwa mwema sana kwa kila mtu basi kila mtu atakuwa mwema sana kwako lakini inakuwa kinyume chake.

Kuwa mvumilivu sana, mnyenyekevu kupitiliza,mwenye kusamehe makosa mara kwa mara kutafanya wakati mgumu sana kwako kukemea tabia mbaya za watu ambao unajitoa mhanga kuwafurahisha na madhara yake Watu ambao unajitoa mhanga kuwafurahisha watafanya makosa makubwa sana kwa makusudi kabisa kisha wanageuza kibao kwako.

3.UTAFICHA NA KULEA TABIA MBAYA ZA WAPENDWA WAKO

Kama utakuwa mzazi au mlezi ambaye upo na sifa za upole kupitiliza, huruma, kunyenyekea, kusamehe makosa,kutaka kumuelewa kila mtu,kutaka kumsaidia kila mtu ghafla utajikuta marafiki zako,watoto wako na mwenza wako wapo na tabia zenye kupigwa vita katika jamii lakini hauna ujasiri wa kukemea tabia hizo.

Wapendwa wako wanaweza kutumia fedha nyingi sana bila sababu,watafanya makosa makubwa sana mara kwa mara,utapigwa faini kwa uzembe na makosa ya wapendwa wako.

Hofu ya kusemwa vibaya,hofu ya kusemwa upo na roho mbaya,hofu ya kuitwa mchoyo, mbinafsi n.k itakufanya ukubali mambo kwa shingo upande ili kuepuka migogoro, utabeba majukumu mengi sana kuliko uwezo wako ili uepuke migogoro.

Madhara mengine ni

Utakaribisha watu wenye nia mbaya ya kukuangamiza ambao watatunga stori za uongo kuwa wapo matatizoni na watadai wanataka MSAADA wako. 

-Watafanya hivyo kwa sababu wanajua upo na huruma sana.

-Utakuwa na idadi kubwa sana ya watu ambao wanakutegemea, Watu wengi watakuwa wanaishi kwa kutegemea wema wako na pale ambapo utakuwa hauna uwezo wa kujitoa mhanga kwao wanaondoka na kukuacha mpweke kwa maana upendo wao kwako ni pale ambapo watakuwa na shida ya kukutumia tu.

-Utajenga mazoea ambayo hayana mipaka - utashindwa kukataa maombi ya watu wengine lakini utakuwa na wakati mgumu sana kuomba msaada kwa watu wengine kwa kuhofia utaonekana mzigo kwao.

-Utakuwa hauna misimamo,utashindwa kuheshimu maamuzi yako , Watu watakuwa na matarajio ya kupokea kitu kutoka kwako.

-Watu watakupuuza nyakati za sherehe na watakukumbuka kwenye matatizo tu.

-Utashindwa kudai haki zako kutoka kwa watu ambao unajitoa mhanga kuwafurahisha kwa kuhofia utaonekana mbaya.

NINI CHA KUFANYA MBADALA

Zingatia yafuatayo

1.KUWA MWEMA SANA KATIKA JAMII SIYO GUARANTEE YA KUPENDWA WALA SIO KINGA YA MATATIZO

Kama utakuwa na sifa za upole, huruma, kujali, kunyenyekea, kusamehe makosa kupitiliza tambua kwamba sifa hizo sio GUARANTEE ya kupendwa, kusifiwa,kupewa zawadi,kuitwa majina mazuri,kuungwa mkono kipindi kigumu.

Vilevile sifa hizo nzuri sio kinga dhidi ya kukosolewa,kusemwa vibaya, kudhalilishwa hadharani, kufanywa kichekesho, kugombezwa, kukaripiwa, kutolewa dosari za muonekano, kunyimwa msaada, kusalitiwa, kuibiwa, kudhulumiwa, kutapeliwa,kupata kesi, kuzushiwa kashfa za uongo,kusambaziwa umbea,kuachwa mpweke.

Badala yake utabaki ni binadamu kama walivyo binadamu wengine.Utabaki katika kumbukumbu mbaya kwa baadhi ya watu na vilevile utabaki katika kumbukumbu nzuri kwa baadhi ya watu bila kujali utaongea au kufanya kitu gani katika jamii.

Hivyo basi sifa hizo nzuri zisiwe kikwazo cha kufanya maamuzi magumu pale ambapo utaona mfululizo wa matukio yenye udhalilishaji,kuvunjiwa heshima.

Onyesha huruma, upole,kujali, kunyenyekea kusamehe makosa pale ambapo panahitajika siyo kila sehemu au kwa kila mtu.

Ukikutana na mtu mwenye sifa nzuri onyesha sifa hizo nzuri muwe marafiki na endapo imekitaka na mtu mwenye sifa mbaya kama ubabe, ukatili, udikteta, udhalilishaji, dharau, majivuno, kiburi na jeuri simama imara kama kiongozi shupavu ili asije kutumia sifa zako nzuri kama UDHAIFU wako.

Badilika kuendana na mazingira sio kuishi kwa mtindo uleule mbele ya kila mtu.

Kama tatizo lako ni kubwa zaidi tunaweza kuwasiliana kwa ajili ya Counselling session na ufafanuzi wa kilichoandikwa hapo juu na utaona mabadiliko na kujisikia nafuu ndani ya muda mfupi baada ya mazungumzo.(Counseling kwa njia ya simu gharama Tshs 30000 , kuonana uso kwa uso Tshs 40000.

Kwa wapenzi wa kusoma vitabu unaweza kupata nakala zangu orodha ipo chini 👇

Kupata kitabu cha

1.JINSI YA KUPONA MAUMIVU MAKALI SANA MOYONI - (Softcopy Tsh 30000)

2.UTULIVU WA AKILI KIPINDI KIGUMU (Softcopy)

3.FIKRA ZAKO FURAHA YAKO (softcopy)

4.TIBA YA MSONGO WA MAWAZO (by & Softcopy)

5.MALEZI YA UBONGO KISAYANSI( hardcopy & softcopy)

6.TABIA ZA WATU WALIOFANIKIWA (Hardcopy & softcopy)

7.MISINGI 10 YA FURAHA SIKU ZOTE (hardcopy &softcopy)

8.BADILI FIKRA ZAKO BADILI MAISHA YAKO

BEI Kitabu kimoja softcopy 5000 isipokuwa kitabu namba 1 bei yake ni Tsh 30000, hardcopy moja 10000

Mawasiliano

+255766862579
+255622414991

Imeandikwa na Psychologist
Said Kasege
Temeke,Dar es salaam

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news