RUVUMA-Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wameonesha moyo wa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na juhudi za Rais za kuhakikisha mambo muhimu manne yanatekelezwa kwa vitendo nchi.
Mambo hayo ni kuendeleza Umoja, Amani, Mshikamano na kuifungua nchi kiuchumi huku akitekeleza kwa ufanisi Falsafa yake ya 4R.
Katika uongozi wake, Rais Dkt.Samia anaamini katika kile kinachojulikana kama 4R ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconcilation (Maridhiano), Resilience (Ustahamiliivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuidlding (Kujenga Upya).
4R za Rais Dkt.Samia zimeleta mafanikio makubwa kwenye uongozi wake tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.
Leo Septemba 26,2024 Rais Dkt.Samia akizungumza na wananchi wa Kata ya Likola, Wilaya ya Namtumbo, aliposimama eneo hilo kwa ajili ya kuwasalimia akielekea Tunduru, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Ruvuma ameendelea kuwashukuru wananchi kwa upendo mkubwa wanaomuonesha.
Mhe. Rais Dkt. Samia pia,ameendelea kusisitiza kauli yake ya kuwashukuru wakulima wa Ruvuma na maeneo yote nchi nzima kwa jinsi juhudi zao zinavyoendelea kuifaharisha nchi kwa usalama wa chakula huku ziada ikitunzwa, nyingine kuuzwa nje ya nchi na kuwa mojawapo ya vyanzo vya pato la taifa na mapato ya fedha za kigeni.
Mbali na kuwashukuru kwa juhudi na ushirikiano wa wakulima, Mhe. Rais Dkt. Samia pia amesisitiza kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi anayoiongoza, itaendelea kutimiza wajibu wake kuwahudumia wakulima hao, hasa kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo, zikiwemo mbolea, huduma za ugani, mbegu bora na masoko ya mazao yao, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025.