NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amezindua jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbinga mkoani Ruvuma.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amefanya uzinduzi huo leo Septemba 25,2024 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma ambayo inajumuisha matukio mbalimbali ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
"Niipongeze sana Halmashauri ya Mbinga kwa kukamilisha ujenzi huu wa jengo hili, ni jengo nzuri. Nimeingia ndani kuangalia ujenzi unaridhisha sana, na ni jengo lenye nafasi za kutosha kwa hiyo niwashukuru sana.
"Lakini, pamoja na hilo nishukuru sana na nipongeze madiwani, mmesimamia ujenzi wa jengo hili, lakini pia mmewaza kuwa na jengo la kitega uchumi, jengo la kuwawezesha wananchi, hongereni sana.
"Nimuombe Mungu awatie nguvu mlimalize jengo hilo na lifanye kazi iliyokusudiwa, kukamilika kwa jengo hili ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imetutaka tujenge majengo ya halmashauri ili kutoa nafasi ya kuhudumia vizuri wananchi.
"Lakini, pia kukuza utawala bora,nimeambiwa nilipokuwa nikizungumza na Mkurugenzi kwamba kabla ya jengo hili, Mkurugenzi alikuwa kwake, wakuu wa idara walikuwa kwao, ofisi nyingine zilikuwa kwao.
"Lakini, baada ya kukamilika jengo hili, maofisi yote, wakuu wa idara na kila mtu yuko huku ndani, kwa maana hiyo huduma zote zinatolewa ndani ya jumba moja ili kuharakisha huduma kwa wananchi, lakini pia kuleta utawala bora, kwamba haki za wananchi zinashughulikiwa haraka iwezekanavyo na zote ni pahali pamoja,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, mpaka sasa majengo ya utawala ya halmashauri 67 ujenzi wake umekamilika.
Vile vile, Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema,majengo mengine 60 ya halmashauri yapo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji nchini.
"Mheshimiwa Rais, ulipoingia tu madarakani ulitoa shilingi bilioni 206.24 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala ya halmashauri, nyumba za wakurugenzi pamoja na nyumba za wakuu wa idara ili kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wananchi.
"Ninapenda kukufahamisha kuwa, mpaka sasa majengo ya utawala 67 yamekamilika na sasa wananchi wanapata huduma karibu kabisa na maeneo yao."
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura Rwiza amesema, jengo hilo limegharimu shilingi bilioni 3.2 kati ya shilingi bilioni 3.5 zilizokua zimetengwa na kiasi kikichobakia ni kwa ajili ya kazi ndogo ndogo zilizobakia.
“Mheshimiwa Rais jengo hili la halmashauri lina jumla ya ofisi 72 kwa ajili ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi, Wakuu wa Idara pamoja na wasaidizi wao wote, na zaidi kuna kumbi mbili za mikutano kwa ajili ya mikutano ya vikao vya menejimenti na vile kamati pamoja na Baraza la Madiwani."
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ni miongoni mwa halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 ina wakazi 285,582 kati yao wanaume ni 141,271 sawa na asilimia 49.5 na wanawake ni 144,311 sawa na 50.5 ya idadi hiyo.