Prof.Chibunda ataja uhusiano uliopo kati ya SUA na Hayati Sokoine

NA GODFREY NNKO

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda amesema, kuna uhusiano mkubwa kati ya chuo hicho na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine.
Prof.Chibunda ameyasema hayo leo Septemba 30,2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) ambacho kinazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Pia, amesema kuwa, wataalamu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine wameshiriki kikamilifu kukiandika kitabu hicho ikizingatiwa kuwa, chuo hicho ni cha kipekee nchini kwa kupewa jina la kiongozi wa nchi.

Akielezea kuhusu uhusiano wa chuo hicho na Edward Moringe Sokoine, Prof.Chibunda amesema kuwa, "Kumbukumbu zilizopo zinaonesha kwamba, tarehe 11 Aprili, 1984 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilijadili Muswada ambao ulikuwa na dhumuni la kuanzishwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Morogoro.

"Kwa kupandisha hadhi kilichokuwa Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, itakumbukwa pia kwamba mjadala kwenye kikao hicho cha Bunge ulikuwa mkali na mgumu kwani, baadhi ya wabunge hawakutaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kigawanywe.

"Ni kutokana na umahiri mkubwa wa kushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine na imani yake ya dhati kwamba ili kilimo katika nchi yetu kiweze kuimarika nchi yetu ilihitaji chuo kikuu mahususi cha kilimo ndipo muswada ulipita na kuwa sheria.

"Aidha, itakumbukwa kwamba kesho yake yaani tarehe 12 Aprili, 1984 Edward Moringe Sokoine alifariki dunia kutokana na ajali ya gari."

Prof.Chibunda amesema kuwa,baada ya kifo chake uongozi wa chuo wakati huo kwa kutambua mchango mkubwa wa Edward Sokoine katika kuanzisha chuo chao waliomba Serikali jina la Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro libadilishwe na kuwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
"Ili kuendelea kuenzi kazi na michango yake katika chuo chetu na imani yake kubwa katika kilimo na katika maendeleo ya nchi yetu, tunaendelea kuishukuru Serikali,kwamba iliridhia ombi hilo na kuwasilisha bungeni muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya jina hilo.

"Na baadaye kuidhinishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na jina hilo lilianza kutumika rasmi ilipofika tarehe 1 Julai, 1984."

Amesema, ili kuendeleza kumuenzi na kuendeleza fikra za Hayati Sokoine tangu mwaka 1992 Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kimekuwa kikiandaa kila mwaka muadhara wa kumbukizi wa kumkumbuka Hayati Edward Sokoine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news