DAR-Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameishauri sekta binafsi kutumia fursa ya upatikanaji mdogo wa huduma ya utengamao kushirikiana na serikali kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wingi nchini.
Profesa Mkenda aliyasema hayo Septemba 18,2024 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama alipokuwa akifungua Kongamano la pili la utengamao nchini lililoandaliwa na Taasisi ya Rehab Health ikishirikiana na wadau wengine.
Alisema, uelewa kuhusu upatikanaji na umuhimu wa huduma za utengamao nchini bado ni mdogo huku wengi wakidhani kwamba maeneo ya mazoezi ya viungo ndio vituo vya kutolea huduma za utengamao.
“Kutokana na sababu hiyo nipende kusema kwamba hii ni fursa kubwa kwa sekta binafsi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha huduma za utengamao zinapatikana kwa wingi, nipende kuipongeza taasisi ya Rehab Health kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii juu ya huduma za utengemao,” alisema Profesa Mkenda.
Alisema upo upungufu wa rasilimali watu katika eneo la utengamao na kwa asilimia kubwa zinapatikana katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda pekee.
“Kulingana na Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika, hadi kufikia Agosti 2024 Tanzania ilikuwa na wataalamu 671 wa tiba ya fiziotherapia, wataalamu 158 wa tiba kwa vitendo, wataalamu 125 wa viungo tiba na vifaa vya tiba saidizi na wataalamu sita wa huduma za matamshi,” alifafanua.
Aliongeza kuwa ili kushugulikia upungufu wa rasilimali watu katika huduma za utengamao, kozi ya shahada katika tiba kwa vitendo na huduma za matamshi imeanzishwa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) katika mwaka wa masomo 2023-2024.
“Lengo la serikali ni kuendelea kuboresha vituo vya kutolea hudma za afya ili ziweze kutoa huduma za utengamao ambavyo kwa sasa havitoi huduma hiyo hasa vinavyotoa huduma za msingi,”alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Rehab Health, Remla Shirima alisema kuwa licha ya huduma za utengamao kuendelea kutolewa nchini kwa zaidi ya miaka 70 bado jitihada zinahitajika ili kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma hizi.
Aliipongeza serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuanzisha kitengo chini ya idara ya huduma za tiba ambayo inasimamia huduma za utengamao na kuwa tangu kuanzishwa kwake zimeshuhudiwa hatua madhubuti za serikali ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 huduma za utengamao zimakuwa kipaumbele cha Wizara katika bajeti yake.