ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hatua ya kuanzisha bima ya afya kwa watalii inalenga kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuandaa mazingira salama na rafiki kwa wageni wanaokuja nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 26, 2024 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Balozi mpya wa Italia nchini, Mhe.Giuseppe Sean Coppola aliyefika kujitambulisha.
Aidha,Rais Dkt. Mwinyi amesema bima ya afya kwa watalii sio jambo geni kwani mataifa mengi duniani tayari wamekuwa na huduma hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inamjengea mtalii uhakika wa kupata huduma bora za afya, ulinzi wa ustawi wake ikiwemo kumuondoshea usumbufu anapopata tatizo lolote ikiwemo kupoteza mizigo yake au hati za kusafiria.
Amefafanua kwamba,Serikali imekua ikibeba mzigo mkubwa wa gharama kwa wageni wanaoingia nchini hasa wanapougua, ajali wakati wengine vifo, hivyo ameeleza kuanzishwa kwa bima hiyo kutaipa Serikali unafuu.