Rais Dkt.Mwinyi aipongeza Oman kwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo Zanzibar

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Serikali ya Oman kwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo hapa nchini.

Ni kupitia taasisi mbalimbali za nchi hiyo ambazo zinaunga mkono Zanzibar kiufundi na kitaalamu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 23,2024 Ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia masuala ya Utawala na Fedha, Khalid Almuslahi.

Aidha,Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajenga hospitali kubwa ya mkoa katika maeneo ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambayo itafadhiliwa na Serikali ya Oman.

Rais Dkt.Mwinyi amemhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba uhusiano uliopo baina ya Zanzibar na Oman ni imara, na miradi ya ushirikiano inayoendelea itaendelea kuweka alama muhimu katika kudumisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili.

Vilevile amesema Mji Mkongwe wa Zanzibar, ni eneo muhimu la urithi linalohitaji kuendelezwa wakati wote. Hivyo, juhudi zinazofanywa na Serikali ya Oman za kuukarabati na kuuimarisha ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kuinua uchumi wa nchi.

Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi amesema kwamba, mbali na Mji Mkongwe kuwa kivutio cha utalii, pia ni eneo muhimu kwa kukuza uchumi na utamaduni wa Zanzibar, na Serikali itaendelea na juhudi mbalimbali za kuutunza mji huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news