Rais Dkt.Mwinyi ataka ufumbuzi changamoto za kimazingira

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezitaka wizara zenye dhamana ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufanya kazi kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi changamoto za kimazingira na mabadiliko ya tabianchi zinazoibuka maeneo mbalimbali ya nchi.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji aliyeambatana na timu ya watendaji wakuu wa wizara hiyo, waliofika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, ni vyema wizara hizo mbili kuweka mkazo katika kuzipitia sera, kanuni miongozo, mipango na mikakati ya kudhibiti changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu na kuibua utatuzi wa masuala hayo.

Amesema, uvamizi wa majichumvi kwenye maeneo ya kilimo, visima na makaazi ya wananchi, mporomoko wa fukwe za bahari na ukosefu wa mvua na mvua zisizotarajiwa bado ni matatizo yanayoathiri kwa kiasi kikubwa.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka watendaji wa wizara hizo kutumia makongamano na mikutano ya kimataifa ya kimazingizingira kuziwasilisha changamoto hizo zinaziikabili nchi ili kupata ufadhili na rasilimali za kukabiliana nazo.

Aidha, amewasisistiza kuwa na mipango shirikishi kuanzia ngazi za chini kwa jamii ili nayo itoe mchango wake.

Pia, Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kuzuia athari za mazingira zisiendelee kuathiri maisha ya watu.

Akizungumzia masuala ya Muungano, Rais Dkt.Mwinyi ameridhia ombi la Waziri Kijaji la kutaka siku tatu kila mwezi kwa watendaji wa wizara hizo mbili kukutana Zanzibar na kuwa na mikutano na wananchi kutoa maoni yao juu ya changamoto za Muungano.

Kuhusu biashara ya kaboni (gesi ukaa), Dkt.Mwinyi amewataka watendaji hao kushirikiana kwa pamoja, kujengeana uwezo na kuwatafuta wataalamu kwani biashara hiyo ni mpya ulimwenguni.

Amesisitiza suala la uratibu wa shughuli za Muungano, kwani sekta zote wanazozisimamia zinahitaji ushirikiano wa karibu ili kuleta ufanisi.

Naye, Waziri Kijaji ameeleza tayari wizara hiyo imeandaa timu ya wataalamu na imeanza utafiti na kuandika miradi kwa lengo la kuiwasilisha kwa wafadhili ili kupata fedha zitakazoendesha miradi ya kimazingira.

Amebainisha kuwa, uharibifu wa mazingira ni mkubwa hasa katika fukwe unaosababishwa na mmongonyoko na uvamizi wa maji chumvi katika maene ya kilimo, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kukabiliana na hali hiyo.

Waziri Kijaji amefika Ikulu kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Julai 3, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news