ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Uingereza kwamba Zanzibar inaendelea na mikakati na juhudi kubwa ya kuhakikisha inadhibiti na kuumaliza ugonjwa wa trakoma hapa nchini.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) aliyepo Zanzibar kwa ziara ya siku sita Tanzania kutembelea miradi mbalimbali ya afya inayotekelezwa na taasisi tofauti ambazo yeye ni mlezi wake.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hatua iliyofikiwa na Zanzibar ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali inatokana na juhudi kubwa na misaada ya Afya inayotolewa na Uingereza na kumuahidi kuwa Zanzibar itaendelea kufanyakazi kwa juhudi zaidi ili kupambana na magonjwa hasa yasiyoambukiza (NCDs) yanayoathiri ustawi wa jamii.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kufarajika kwake kwa misaada ya mafunzo ya kitaalamu ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Sekta ya Afya hasa katika kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza yanayotolewa na nchi hiyo ambayo yamekuwa kichocheo muhimu cha kuleta mafanikio kwenye sekta ya Afya na kusisitiza misaada hiyo kuendelezwa.
Dkt. Mwinyi alimuhakikishia Princess Sophie kuwa Zanzibar inaendelea kuweka mkazo zaidi na kuhakikisha huduma bora za sekta ya Afya hususan kuimarisha huduma za kitengo cha uzazi kwa mama na mtoto na kuwataka wafadhili na washirika wengine wa Maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Naye, Princess Sophie ameipongeza Zanzibar kwa hatua iliyofikia katika kuudhibiti ugonjwa wa ‘trachoma’ kwa kiasi kikubwa na kufikia mapema malengo yaliyowekwa na Jumuiya ya Madola (Commonwealth) ya kumaliza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Amesema, Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mfano zilizofanikiwa kuudhibiti na kuutokomeza ugonjwa huo ambao umekua tishio kwa nchi nyingi barani Afrika pia aliisisitiza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha ugonjwa huo haujirudii kwa namna yoyote.
Ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya miradi inayoungwa mkono na nchi yake kwenye sekta ya Afya na kumhakikisha Rais Mwinyi kwa taasisi zote zinazoendesha miradhi hiyo, kuendelea na misaada yake.
Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) ni Mke wa mtoto wa mwisho wa aliyekua Malkia wa Uingereza, Elizabeth II, Prince Eduward ambaye ni mdogo wa Mfalme wa sasa wa Uingereza, Charles III.