ZANZIBAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameutaka Umoja wa Vijana wa Chama wa Cha Mapinduzi (UVCCM) kuweka mikakati maalum ya kuhakikisha wanachama wa chama hicho wanajiandikisha kwa wingi na kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 28, 2024 huko Tunguu, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, wakati wa Mahafali ya Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Zanzibar yaliyoandaliwa na UVCCM katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein (SUZA).
Aidha, ameutaka umoja huo kuhakikisha wanachama wao wote wanajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ifikapo Januari 2025, kwa kuwahamasisha wale ambao bado hawajajiandikisha.
Halikadhalika, amewahimiza vijana kuendelea kuwa raia wema, wenye nidhamu, uzalendo, pamoja na kufuata mafunzo na malezi waliyoyapata kupitia walimu wao wa UVCCM.
Rais Dkt. Mwinyi amewaasa wanafunzi hao kuepuka kujiingiza au kushirikiana na watu waovu wenye nia mbaya kwa maendeleo na badala yake wawe walinzi wa amani na umoja wa Taifa letu.
Pia, Dkt. Mwinyi aliwaahidi viongozi wa UVCCM na vijana wote kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa kuwashirikisha katika masuala ya maendeleo, ikiwemo uongozi.